27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JET YAWAJENGEA UWEZO WAANDISHI WA HABARI

 

Na Sidi Mgumia, aliyekuwa Bagamoyo

‘INFORMATION is power’…hii ni nukuu ya kiingereza ambayo tafsiri yake isiyo rasmi ni kuwa taarifa ni nguvu.

Kwa kuitazama nguvu ya taarifa, Chama Cha Waandishi wa Habari za Maizngira (JET), imeiona haja ya kuwajengea uwezo wasambaza taarifa (Waandishi wa Habari) ili wajue kwa weledi namna sahihi ya kuripoti masuala yote yanayohusu uihifadhi na hifadhi zenyewe.

Bila kujali nani ni nani uhai wa viumbe hai na hasa wanyamapori ni jambo linalomuhusu kila mwananchi.

Wanyapori wanayo faida kubwa kwa jamii na nchi kwa ujumla, mbali ya kuwa kivutio cha utalii, pia ni hazina kwa Taifa.

Ili kuhakikisha wanyapori wanaendelea kuwa na tija kwa nchi na wananchi wake, JET imedhamiria kitafanya kila iwezalo kuhakikisha vizazi vijavyo vinarithi hazina hiyo.

JET haitaweza kushika bunduki na kuingia msituni kuwasaka majangili na wahuni wengine, inachokiweza ni kuhakikisha inatumia kalamu kuendesha mapambano dhidi ya utunzaji wa mazingira, hifadhi na wanyamapori.

Hayo yatafanikiwa kwa sababu ya chama hicho kuwa na hazina kubwa ya wanahabari wenye moyo na dhamira ya kweli ya kutetea na kupigania rasilimaliz a Tanzania na ndio hao waliopatiwa mafunzo hayo maalum.

Mafunzo hayo yaliyokuwa ya siku tatu yalifanyika Bagamoyo mkoani Pwani, yakishirikisha wandishi wa Habari takriban 30, walionolewa na wanahabari wabobezi wa masuala ya uhifadhi.

JET iliendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani USAID chini ya mradi wake wa PROTECT.

Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, aliwaambia wanahabari walioshiriki mafunzo hayo kuwa lengo kubwa la mafunzo ni kuwajengea uelewa mpana wa namna ya kuripoti masuala ya uhifadhi.

Mbali na hilo, Chikomo alisema wanahabari wanayo dhima ya kuutangaza utalii ili uweze kueleweka kimataifa pamoja na kushawishi sekta binafsi kuwekeza kwenye eneo hilo.

“Matarajio yetu baada ya mafunzo haya ni kuwa waandishi watakuwa na uelewa mpana kuhusu uhifadhi wa mazingira na wanayama pori na pia watapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwa kutembelea hifadhi za wanyamapori,” aliongezea Chikomo

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria watetezi wa Mazingira (LEAT) Stanislaus Nenyemba, alisema kuwa kwa kifupi sheria za wanyamapori zina mapungufu haswa katika upande wa fidia, endapo mtu atadhurika katika hifadhi na kusisistiza kuwa ni vyema kuwepo na usimamizi mzuri wa sheria na kanuni kwakuwa hiyo italeta uhusiano bora kati ya wasimamizi wa sheria na jamii zinazozunguka hifadhi, hakutakuwa na uonevu.   

Akiongelea suala la Uwekezaji Kimataifa, mtoa mada Raziah Mwawanga ambaye ni Ofisa Mradi kutoka Taasisi ya Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF), alisisitiza kuwa ni vyema kuwatumia wanyama kama kitega uchumi, lakini na kuwa wanapolindwa hao wanyama ni kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Ukiangalia Tanzania tuna aina mbalimbali za rasilimali ambazo hazipatikani popote duniani, hivyo tunapozilinda hifadhi tunajiongezea uhakika wa kuwa na rasilimali bora na zenye kuvutia kitaifa na kimataifa, kwa mfano tukizuia uvuvi haramu kuna nafasi kubwa ya kuwa na samaki wengi watakao ibua utalii wa samaki,” alisema Mwawanga

Pia alisema kuwa ongezeko la watu ni changamoto katika uhifadhi wa wanyama pori kwakuwa idadi ya watu Tanzania imeongezeka na kuna maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, vitu ambavyo hufanya ardhi iwe kidogo na kusababisha kuhitajika kwa mipango wa matumizi ya ardhi na sera ya wazi ya kuhifadhi wanyamapori ambapo lazima maeneo yatengwe yakiwemo yale ya wakulima, wafugaji, wanyama na maeneo ya wazi.

Akiongelea ujangili katika hifadhi, Ofisa habari kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), Twaha Twalib amesema wameshafanya vitu vingi kukabiliana na ujangili na majangili wameanza kupungua huku wanyama wakiongezeka ikiwamo kufufua ndege, kununua magari, boti kwa ajili ya kufanya doria ambapo sasa wanafika maeneo mengi nchini tofauti na ilivyokuwa awali.

Mwandishi wa habari mkongwe Atilio Tagalile pamoja na Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), Abdallah Katunzi wamewataka waandishi wa habari kuandika kwa wingi habari za uhifadhi wanyamapori na kuwa watafiti na sio wapasha habari tu  jambo ambalo litawafanya waje na habari mpya au tofauti na wengine.

Vilevile kwa kushirikiana na waandishi wa habari JET pamoja na USAID PROTECT,  wametaka jamii ijengewe uwezo na kuaminishwa kuwa uhifadhi ni maisha ya kila siku kwa mwanadamu na yana faida kubwa kwao.

Lakini pia wanaosimamia masuala ya uhifadhi wahimize haja ya kuzilinda, kuzihifadhi na kuzitumia vizuri rasilimali zilizopo kwa kwa faida za sasa na za baadae.

Wamesisitiza kuwa ni muhimu sana kwa jamii kulinda wanyama pori hususani walio katika hatari ya kutoweka kama jamii ya paka wakubwa.

Hifadhi za Taifa, Tanzania

Maeneo yaliyotengwa kama Hifadhi ya Taifa yanayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni pamoja na hifadhi ya Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, hifadhi ya taifa ya Arusha, Rubondo, Serengeti, Saadani, Tarangire, Udzungwa, Kitulo na hifadhi ya Mkomazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles