26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jeshi Sudan lazua taharuki Al Jazeera wakifungiwa

KHARTOUM, SUDAN

UONGOZI wa kijeshi nchini Sudan umesema kuwa kambi za waandamanaji mjini Khartoum zimekuwa tishio kwa usalama wa taifa, hali ambayo imelilazimu jeshi la nchi hiyo kuagiza kufungwa kwa ofisi za kituo cha habari cha Shirika la  Al Jazeera.

Katika taarifa waliyoitoa kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa baraza la kijeshi, Jenerali Bahar Ahmed Bahar, amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu aliosema waharibifu.

Kwa miezi kadhaa sasa waandamanaji wameendelea kutia ngumu kutoka kwenye maeneo yanayozingira makao makuu ya jeshi, wakishinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

“Eneo la maandamano limekuwa si salama na linahatarisha usalama wa taifa,” alisema Jenerali Bahar Ahmed Bahar, mkuu wa jeshi mjini Khartoum.

Jeshi linasema magari maalumu ya kijeshi ya kikosi maalumu yamekuwa yakishambuliwa na mengine kuzuiliwa na waandamanaji kwenye eneo la maandamano.

Eneo hilo limekuwa kitovu cha vuguvugu la maandamano, ambayo yalishuhudia kuondoka madarakani kwa Rais Omar al-Bashir, aliyeondolewa na jeshi mwezi uliopita, na tangu wakati huo wamekuwa wakitaka wanajeshi nao kukabidhi madaraka kwa raia.

Katika hatua nyingine, mamlaka nchini humo zimekipa taarifa kituo cha habari cha Al Jazeera kufunga ofisi zake mjini Khartoum kwa maelekezo ya baraza la kijeshi, bila hata ya kutoa sababu.

Uamuzi huu wa jeshi unamaanisha pia kunyang’anywa vibali vya kufanyia kazi nchini humo kwa wawakilishi wa kituo hicho pamoja na wafanyakazi wengine.

Shirika la Al Jazeera, lenye makao yake nchini Qatar, limeamriwa na Serikali ya Sudan kuondoka mara moja nchini humo.

Katika taarifa yake, uongozi wa Al Jazeera umekosoa hatua ya baraza la kijeshi, ukisema kitendo hiki ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa watu kutoa na kupata habari.

“Shirika letu linaona katazo hilo kama shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa taaluma ya uandishi wa habari na haki za watu kupata habari, kufahamu, kuelewa hali halisi ya mambo yanayoendelea nchini mwao Sudan,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, Al Jazeera imesema kuwa itaendelea na shughuli zake kama kawaida za kuripoti kinachotokea nchini Sudan, licha ya uhuru wao kuingiliwa na mamlaka ya Sudan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles