24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi lachafua hali ya hewa Sudan

KHARTOUM, SUDAN 

HALI nchini Sudan bado si shwari baada ya jana vikosi ya ulinzi na usalama kutumia nguvu kuvunja mikutano ya watu waliokuwa wakikusanyika na kukaa nje ya Makao Makuu ya Jeshi mjini Khartoum, waandamanaji wamesema.

Milio ya risasi ilisikika jana katika mji wa Khartoum huku ikiripotiwa  watu karibu nane wakiwa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Sudan  imekuwa ikiendeshwa na Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) tangu Rais  Omar al-Bashir aondolewe kwa mapinduzi mwezi Aprili mwaka huu.

Waandamanaji wamekuwa wakikusanyika na kudai utawala wa kiraia uchukue nafasi ya kuongoza nchi na si jeshi.

“Sasa jaribio linafanyika kuwaondoa watu wanaoketi nje ya Makao Makuu ya Jeshi,” ilieleza taarifa fupi iliyotolewa na Chama cha Wanataaluma wa Sudan,  kundi ambalo linaongoza kwa kuhamasisha maandamano nchi nzima.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema matairi na vizuizi vilikuwa vikichomwa na waandamanaji waliokuwa wakijaribu   kupambana na vikosi hivyo vya ulinzi.

Mwandishi wa habari, Benjamin Strick, ambaye ni mtaalamu wa kuthibitisha kwa video kupitia akaunti ya Twitter, aliweka video ya aina yake kutoka Khartoum,  iliyokuwa ikionesha jinsi milio ya risasi ya kujirudiarudia inavyoweza kusikika.

Pamoja na hayo, jeshi la Sudan halijatoa taarifa yeyote wala kueleza chochote kwa umma.

Waandamanaji walikuwa wakizingira  uwanja katika eneo la mbele la makao makuu ya jeshi tangu Aprili 6  mwaka huu, siku tano kabla ya Bashir kuondolewa madarakani.

Mwezi uliopita, waandamanaji na watawala walitangaza kwamba wamekubaliana juu ya muundo mpya wa uongozi na miaka mitatu ya kipindi cha mpito kuelekea kwenye utawala wa kiraia.

Lakini bado walikuwa wanahitaji kuamua juu ya muundo wa kile kinachoitwa baraza huru, ambalo litakuwa mamlaka makubwa ya kufanya uamuzi katika kipindi cha mpito.

Lakini inaelezwa hawawezi kukubaliana kama raia au wanajeshi wanapaswa kuwa na nafasi nyingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles