24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu China kuiyumbisha Marekani kwa madini

BEIJING, CHINA

DALILI zinaonesha kuwa huenda China ikadhibiti usafirishwaji wa madini yake ya kipekee na adimu yanayofahamika kwa lugha ya kiingereza kama ‘rare earths’ kwenda Marekani katika kipindi hiki mzozo wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili ukizidi kufukuta.

Madini hayo kutoka China ni malighafi kuu ambayo hutumiwa na kampuni nyingi za Marekani kutengeneza vitu kama magari yanayotumia nguvu za umeme, simu na bidhaa nyingine nyingi za kielektroniki.

Mwaka jana utafiti uliofanywa na shirika la Jiolojia la Marekani uliorodhesha madini hayo kama yenye umuhimu mkubwa katika uchumi na ulinzi wa taifa la Marekani.

“China inatathmini hatua ya kuthibiti usafirishwaji wa madini hayo ya kipekee nchini Marekani,” Gazeti la kitaifa la Global Times, liliandika katika mtandao wake tweeter wiki hii.

Madini hayo ni kundi la madini 17 yanayotumiwa kwa utengenezaji na ukuzaji wa vitu kadhaa katika sekta mbali mbali, ikiwemo nishati mbadala, bidhaa za kielektroniki, bidhaa za kutengeneza mafuta na pia hutumika kutengeneza vioo.

Japo madini hayo husemekana ”hayapatikani” kwa urahisi, utafiti uliofanywa na Shirika la Jiologia la Marekani umebaini kuwa yanapatikana kwa wingi sehemu za mbali zaidi.

Hata hivyo, kuna sehemu chache sana duniani kunakopatikana migodi inayotoa madini hayo.

Uchimbaji wake  unaelezwa ni mgumu na umetajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

China ndio kinara wa uzalishaji wa madini hayo kwa kutoa asilimia 70.

Myanmar, Australia, Marekani na mataifa mengine pia huchimba madini hayo kwa kiasi kidogo.

Mwaka jana karibu asilimia 90 ya uchakatwaji wa makinikia yake ulifanyika nchini China.

Kampuni moja ya Australia inayoendesha shughuli zake nchini Malaysia ilichakata kiasi kilichobaki.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kiwango cha uzalishaji wa madini hayo ya kipekee kilichosafirishwa nje ya China kiliongezeka mara mbili zaidi kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na nchi hiyo.

Takwimu za Serikali ya Marekani zinabainisha kuwa; Marekani inaagiza karibu asilimia 80 ya kundi la madini hayo 17 ya kipekee kutoka China.

Estonia, Ufaransa na Japan pia zinaiuzia Marekani madini hayo japo kwa uchache.

Kampuni pekee inayosafisha madini hiyo nchini Marekani hutuma malighafi yake China kusafishwa – na tayari imeathiriwa na nyongeza ya kodi ya asilimia 25 iliyowekwa na China.

Marekani inaweza pia kuagiza madini hayo kutoka Malaysia, lakini sio kwa kiwango kitakachokidhi mahitaji yake.

Serikali ya Malaysia imetishia kupiga marufuku uchakatwaji wa madini hayo kutokana na sababu za kimazingira.

Kutokana dalili hizo za China, wengi wamenza kujiuliza iwapo Marekani inaweza kuchakata madini hayo pasipo kuitegemea China.

Hata hivyo,  jambo hilo linaelezwa kuwa linaweza kuichukua muda mrefu kwa sababu itakabiliwa na changamoto ya kupata malighafi ikiwa China itaondolewa katika mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa hiyo kwenda Marekani.

Hadi mwaka 1980, Marekani ilikuwa ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini hayo.

China ishawahi kudhibiti usafirishaji wa madini hayo hapo kabla.

Mwaka 2010, walichukua hatua hiyo dhidi ya Japan, kutokana na mzozo wa kimaeneo uliokuwepo.

Inaelezwa kuwa ikitokea China ikaidhinisha hatua ya kudhibiti uuzaji wa madini yake, kampuni nyingi za Marekani zinazotegemea madini hayo kuendesha biashara zao zitapoteza matrilioni ya dola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles