Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi limesema matukio ya kupotea na kuibiwa kwa watoto yamepungua ambapo takwimu zinaonesha kwa kipindi cha mwaka 2018 kulikuwa na matukio 116 ukilinganisha na mwaka 2017 ambao matukio 136 yaliripotiwa na kufanya pungufu ya matukio 18 ambayo ni sawa na asilimia 13.4.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Jeshi hilo DCP Ahmed Msangi leo Jumatatu Januari 21, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea hali ya usalama ilivyo nchini, ambapo amesema matukio ya watoto kuibiwa na kupotea yaliibuka 2017 hali iliyoleta hofu kwa jamii hasa wazazi na walezi nchini lakini hali hiyo ilidhibitiwa kikamilifu.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa matukio ya mauaji yanayotokana na ulevi yaliyoripotiwa nayo yamepungua kutoka 129 mwaka 2017 hadi kufikia 118 mwaka jana, ikiwa ni pungufu kwa matukio 11 sawa na asilimia 8.5.
“Pamoja na kupungua kwa matukio haya ya kupotea kwa watoto Jeshi la Polisi tunatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutowaacha watoto wao kutembea peke yao ama kwenda sehemu hatarishi bila uangalizi wa watu wazima, pia kuwa makini na watu wasiowafahamu kwa kutowaachia watoto na kutomuamini kila mtu, ” amesema.
Aidha amesema pamoja na takwimu za mauaji yatokanayo na pombe kupungua, wanatoa wito kwa watumiaji wa vileo kunywa kwa kiasi na kujiepusha na vitendo vya vurugu pindi wanapokuwa wamelewa.