NAIROBI, KENYA
Jeshi la Polisi nchini Kenya limetangaza kutoa dola za kimarekani milioni 10 ambazo ni sawa na milioni 23 na nusu fedha za kitanzania kama zawadi kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Silvia Romano ambaye ni mfanyakazi wa kujitolea wa kutoa misaada mwenye asilia ya Italia.
Silvia (23) alitekwa na watu wenye silaha akiwa katika moja ya hoteli katika kata ya Kilifi kusini-mashariki mwa nchi hiyo, huku watu watano wakiwamo watoto watatu, walijeruhiwa katika shambulio hilo la kumteka na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
Jeshi la Polisi limesema kuwa linafanya kila linalowezekana kuhakikisha Silvia anapatikana na watekaji wake wanatiwa nguvuni.
Bado haijafahamika wazi sababu za kutekwa kwa mfanyakazi huyo wa kujitolea, aliyetekwa na wahuni wa mtaani, lakini pia inasemekana kuwa watekaji wanaweza kuwa na uhusiano na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabab.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, Joseph Boinett, mpaka sasa watu ishirini wamekwisha kamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo.
Silvia ni mfanyakazi wa kujitolea katika shirika la Kiitalino la Africa Milele Onlus, ambaye ni mfanya kazi wa kwanza kutoka katika shirika la kigeni kutekwa nchini Kenya tangu nchi hiyo kukumbwa na kipindi cha mpito cha matukio ya utekaji nyara yaliyokuwa yamekithiri na kutishia sekta ya utalii kuporomoka mnamo mwaka 2011.