-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge,Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenister Mhagama ametoa siku saba kwa taasisi za serikali, wizara, makampuni na watu binafsi kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Kutokana na hali hiyo ameiagiza bodi za wadhamini za mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kuhakikisha wanawasukuma wadeni wao kulipa madeni yote wanayodaiwa ili kuiwezesha mifuko hiyo kujiendesha kwa ufanisi zaidi.
Tamko hilo alilitoa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni  ambapo alitumia fursa hiyo kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake anayeshughulikia Kazi naAjira, Erick Shitindi, kuhakikisha uongozi wa mifuko unampatia ripoti ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wadeni wote walioshindwa kulipa madeni yao.
“Ninafahamu fika kuna mikataba ambayo ilisainiwa na pande zote mbili kabla ya kutolewa kwa hiyo mikopo na makubaliano mengine hivyo naomba basi mikataba hiyo itumike kufanikisha agizo hili,’’ alisema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema licha ya mfuko wake kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo majengo bado wateja wake wengi hawajalipa madeni wanayodaiwa na mfuko huo ikiwemo watu binafsi, taasisi za serikali na zile binafsi wakiwemo pia wale walionunua nyumba za shirikal hilo.
Alisema shirika hilo bado linadai takribani Sh bilioni 20 kutoka kwa wa wapangaji wake deni linalohusisha pia Dola za Marekani milioni 1.2.
Kiasi kingine cha bilioni 86 kinadaiwa kama adhabu kutoka kwa waajiri walioshindwa kukamilisha makato ya wafanyakazi wao.