24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Majaliwa asimamisha maofisa misitu wanne

kassim-majaliwaNa MWANDISHI WETU, RUFIJI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi maofisa misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani kwa muda usiojulikana baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.

Maofisa waliosimamishwa kazi, ni Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk. Paul Ligonja, Ofisa Misitu wa Wilaya hiyo, Gaudens Tarimo, Ofisa Misitu, Yonas Nyambuya na Ofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) , Seleman Bulenga.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo, kukusanya magogo yote yaliyoko msituni na kuyapiga mnada, huku akiitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji walizozitoa.

Waziri Mkuu Majaliwa alichukua uamuzi huo wilayani hapa jana, alipozungumza na watumishi wa Wilaya ya Rufiji kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye viwanya vya jumba la maendeleo wilayani hapa.

Alisema Wilaya ya Rufiji, ni moja ya wilaya inayoongoza kwa uvunaji wa mazao ya misitu bila kufuata utaratibu licha ya kuwa na maofisa misitu wa kutosha.

“Hakuna mafanikio katika sekta ya misitu kwenye wilaya hii. Nasimamisha shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu pamoja na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha watu wanakata magogo bila kufuata utaratibu.

“Haiwezekani Rufiji iwe shamba la bibi, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa washiriki vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuli ya Kilwa kisha fedha wanatia mifukoni,” alisema Waziri Mkuu.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Rashid Salum, kufuatilia maagizo aliyoyatoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Awali, Mbunge wa Rufiji Mohammed Mchengelwa (CCM), alilalamikia vitendo vya dharau vinavyofanywa na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya hiyo na kusababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles