Na Ibrahim Yassin-Kyela
JENGO wodi ya kina mama katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela, limeungua moto chanzo kikieleza ni hitilafu ya umeme, tukio ambalo limezua taharuki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ezekiel Maghehema, alifika eneo la tukio na kuona hali halisi kisha akawatoa hofu wananchi na kwamba wagonjwa wote wapo salama.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta, alisema tukio hilo lilitokea jana saa tisa jioni, huku akisema bado wanaendelea kufanya tathimini kujua gharama ya vitu vilivyoungua kwani kwa sasa walikuwa na jitihada za kuwahamishia wagonjwa kwenda kituo cha afya Ipinda.
“Nawashukuru wananchi kwa kusaidia kuuzima moto, vitu mbalimbali vimeungua lakini bado tupo kwenye harakati ya kufanya tathimini na wataalamu mbalimbali kujua gharama halisi na tutakapokamilisha tutawapa taarifa halisi juu ya idadi ya vitu na uharibifu uliotokea’’alisema Kitta.
Akizungumza jana na gazeti hili, Athuman Michael mkazi wa Kyela alisema alifika hospitalini hapo kumuona mgonjwa wake, alipofika alishangaa kuona jingo linaungua huku akina mama na wagonjwa wengine wakikimbilia nje kujinusuru.
“Mama mmoja alikimbia akiwa mtupu alikiwa amembeba mtoto, sisi tulimrushia vitenge akajisitili akiwa nje ya jengo na ilipofika gari la kubeba wagonjwa, iliwabeba na kuwahamishia kituo cha Ipinda,”alisema.
Juma Jamal mkazi wa Kyela alisema baada ya kuona moto unaenea katika majengo mengine, walilazimika kuvunja vibaraza vinavyounganisha jengo kwa jengo ili kuzuia moto usienee kwenye majengo mengine.