27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Hata wasichana wa kuanzia miaka 25 wanapata saratani ya matiti – Daktari

Na AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM 

MKURUGENZI wa Huduma za Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa, amesema takwimu za saratani ya matiti zinaonesha kwamba saratani hiyo sasa imeanza kushambulia hadi wanawake wenye umri mdogo tofauti na miaka ya nyuma.

DK Kahesa alisema wastani wa umri wa wanawake wanaogundulika kuugua saratani ya matiti ORCI, umeshuka ambapo mwaka 2008/09 wanawake waliokutwa wakiugua saratani walikuwa wale wa kuanzia wastani wa miaka 64 lakini kwa mwaka 2019, wastani huo ulishuka hadi miaka 56.

“Umri wa miaka 56 ni wastani ambao tumeupata baada ya kujumlisha data zetu, wapo hadi wanawake wenye umri kuanzia miaka 25 ambao tumewakuta na saratani hii, hapa kwenye taasisi yetu,” alibainisha.

Dk. Kahesa alisema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Globalcan za 2018, inakadiriwa zaidi ya wagonjwa 42,060 wa saratani hugundulika kila mwaka Tanzania na kati ya hao asilimia 7.2 ni wa saratani ya matiti.

“Katika uhalisia, takwimu zetu nchini zinaonesha mwaka 2018 wagonjwa wa saratani walioweza kuhudhuria hospitalini ni zaidi ya 12,215 kati ya hao 42,060 wanaokadiriwa.

“Aidha, kati ya hao 12,215 walioweza kuhudhuria wanawake waliopata saratani ya matiti walichukua wastani wa asilimia 16 ya wagonjwa wote.

 “Hapa Ocean Road ambako tunapokea wagonjwa kutoka nchi nzima, mwaka 2018/19 tuliona zaidi ya wagonjwa 7,426 kati ya hao 965 walikuwa wa saratani ya matiti ambao ni sawa na asilimia 13 ya wagonjwa wote tuliopokea.

Dk. Kahesa alisema takwimu za ORCI zinaonyesha saratani ya matiti ni tatizo kubwa ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, baada ya saratani ya kizazi na saratani ya tezidume.

Alisema takwimu zinaonesha kuna hatari ya wanawake 17 katika kila wanawake 100,000 kupata saratani hiyo, ambapo kati ya wanawane 100,000  ambao hupoteza maisha ni 22 hupoteza maisha kutokana na saratani hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo katika kuelekea Oktoba ambao ni mwezi maalum wa uhamasishaji na kutoa elimu juu ya saratani hiyo, wataalamu wa taasisi hiyo wamejipanga kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani hiyo na kufanya uchunguzi wa awali ili kuwagundua mapema wagonjwa.

“Kwa kuwa tunaona wenye umri mdogo nao wanagundulika hivi sasa, tunakusudia kuwafikia moja kwa moja, tutaanza na vyuo viwili na hapa ORCI elimu na uchunguzi wa awali unaendelea kufanyika,” alibainisha.

Alisema saratani hiyo huathiri jinsi zote lakini kwa wanaume ni kwa kiwango kidogo cha asilimia moja tu kwa wanawake ni asilimia 99.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles