Ramadhan Hassan – Dodoma
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kukamilisha kwa wakati miradi inayopewa na Serikali na kuzingatia ubora na thamani ya fedha ionekane.
Agizo hilo alilitoa jana jijini hapa wakati akitoa hotuba kwenye hafla ya ufunguzi wa jengo la makao makuu ya JKT eneo la Buigiri Chamwino.
Alisema Serikali imekuwa ikilitumia jeshi hilo katika miradi mbalimbali, hasa ile ya ujenzi, hivyo lazima wahakikishe inakamilika haraka na kwa ubora.
“Lazima mtekeleze majukumu yenu kwa haraka na ufanisi mkubwa, hii ni sifa kubwa ya kupatiwa kandarasi nyingi zaidi na Serikali,” alisema Jenerali Mabeyo.
Aidha, aliitaka JKT kuzingatia sheria ya manunuzi katika bidhaa ambazo wamekuwa wakizitumia, ikiwa ni pamoja na kununua mahitaji moja kwa moja kwa wazalishaji.
“Inatakiwa vifaa hivi ambavyo mnavitumia katika ujenzi wa miradi hii kuvinunua kutoka kwa wazalishaji, lakini ni lazima tuzingatie taratibu za manunuzi,” alisema Jenerali Mabeyo.
Pia, alilitaka jeshi hilo kutumia fursa wanazopata kutoka serikalini kwa kukabidhiwa miradi mikubwa ya kutekeleza kujiimarisha na kujijengea uwezo, ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vyao kuliko kukodisha.
Aidha alisema Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) yatajengwa kwa kutumia wataalamu wa JKT.
Hivyo aliagiza JKT kujipanga kimuundo, vifaa na kifikra katika kujenga na kukamilisha ujenzi huo wa makao makuu ya ulinzi wa taifa kwa kuzingatia uweledi, matumizi sahihi ya fedha na kuukamilisha kwa haraka.
“Ikumbukwe Novemba 25 mwaka jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa makao makuu ya jeshi, Rais Dk. John Magufuli alitoa Sh bilioni 10 na akasisitiza ujenzi huo tuufanye wenyewe.
“Kutokana na uzoefu mlionao Jeshi la Kujenga Taifa katika kusimamia miradi mbalimbali ya ujenzi, nina imani kazi hiyo mtaiweza,” alisema Jenerali Mabeyo.
Alisema kuwa upo umuhimu kwa JKT kujipanga kimuundo, vifaa, kifikra ili kukamilisha kazi hiyo haraka kwa kutanguliza masilahi ya jeshi na taifa.
Jenerali Mabeyo alisema kwa sasa hatua ya ujenzi wa makao makuu ya jeshi ipo kwenye michoro ambapo alisisitiza michoro ya majengo ya kijeshi ina taratibu zake.
Alisema hatua za ujenzi wa makao makuu ya JKT zilianza Januari 22 mwaka 2018 wakati wa uongozi wa Meja Jenerali Michael Isamuyo, kwa kuundwa kamati ya kutafuta eneo la ujenzi.
Jenerali Mabeyo alimpongeza Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Charles Mbuge kwa kukamilisha ujenzi wa makao makuu ya JKT kwa wakati.
“Naomba myatunze majengo haya kwani kumekuwa na hulka kwa baadhi ya watu kutotunza majengo ya umma kwa sababu fedha hazitoki mifukoni mwao,” alisema Jenerali Mabeyo.