28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JANUARY: WANAOHARIBU MAZINGIRA NZEGA WAKAMATWE

MAZINGIRA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, akipanda mti kuunga mkono jitihada za upandaji miti kwa wakazi wa Kijiji cha Nkiniziwa, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora juzi. Mti huo pia ameukabidhi kwa mtoto Masoud Maganga ili autunze kama kielelezo cha kutunza mazingira. Picha: Mpigapicha Wetu

Na Mwandishi Wetu -Nzega          |             


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, ameiagiza Wilaya ya Nzega, ifanye operesheni kali ya kuwakamata watu wote wanaoharibu mazingira.

Agizo hilo alilitoa mjini hapa juzi alipozungumza na wakazi wa vijiji vya Ngukumo na Mwambaha wilayani hapa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, ya kukagua, kutathimini, kuzungumza na viongozi na wananchi kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira na uanzishwaji na ufuatiliaji utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi Mazingira ya mwaka 2004 katika ngazi za Serikali za Mitaa.

“Ndugu zangu sina budi kuwakumbusha kuwa siku hizi kuna wakimbizi wa mazingira, watu wanaharibu mazingira katika maeneo yao na kuhamia maeneo mengine, jitihada za maendeleo zote hazitakuwa na maana kama hatutatunza mazingira.

“Wakazi wa vijiji hivi kuweni wakali kwa rasilimali zenu na hakikisheni mazingira yanatunzwa kwa sheria kali zaidi,” alisema.

Pia aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuwa na uhifadhi wenye tija ambao wananchi wako tayari kushiriki kwa nguvu zote.

Katika hatua nyingine, aliunga mkono shughuli za maendeleo kwa kuchangia Sh milioni moja za ujenzi wa zahanati na matundu ya choo katika Shule ya Msingi Mwambaha.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngukuwa, alisema changamoto wanayokabiliwa nayo ni uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na uvunaji holela wa misitu na shughuli za kilimo.

Akitoa taarifa kwa January, Ngukuwa alisema: “Wilaya yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wavamizi kutoka mikoa jirani wanaojihusisha na shughuli za ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kilimo kisicho endelevu, kwa kiasi kikubwa wanachangia uharibufu wa mazingira, kwa kuwa hivi sasa Nzega imekuwa soko la mkaa kwa Shinyanga na Mwanza.”

Kuhusu hatua wanazochukua, alisema wanafanya doria za mara kwa mara kijijini hapo kwa kushirikiana na wananchi wenyewe na kubaini wavamizi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles