Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amewasihi wapenzi na mashabiki wake kujiepusha na malumbano yasiyo na msingi hasa wale wanaotumia jina lake kufanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, amewataka kuwa wavumilivu wa mawazo tofauti kwani ndiyo njia pekee ya kupanua demokrasia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, January aliwataka watu wanaompinga kujenga hoja zaidi badala ya kulipiza dhihaka juu yake kwa kutoa dhihaka kwa wagombea wengine au kutoa dhihaka kwa wazee kwa ujumla.
“Hata hivyo, msiache kunisemea pale mnapoona kuna njama za makusudi za kupindisha ukweli juu yangu na juu ya makusudio yangu.
“Kuomba uongozi ni kuomba utumishi, sio mapambano, sio suala la kufa au kupona. Unaomba kibali kwa Mungu kuwaongoza watu wake kupitia ridhaa yao. Tusisahau kumuomba Mungu atupatie kiongozi mzuri mwenye hekima na atakayetenda haki kwa watu wote,” alisema January katika taarifa hiyo.
Julai 3, mwaka huu January, aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kugombea urais mwakani na kueleza kuwa amefikia uamuzi huo kwa asilimia 90.
Makamba alitangaza dhamira hiyo, alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Mahojiano hayo yaliyokuwa yakirushwa kutokea jijini Londoni Uingereza, ambayo yalifanywa na mtangazaji Salim Kikeke, Makamba alisema tayari amekwishajitafakari, kujitathmini na ameridhika kwamba wakati ukifika atachukua fomu za kugombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kutokana na kujitathimini kwake, dhamira imemtuma kwa asilimia 90 kuwania kiti hicho akiwa na lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwatoa walipo.