NA MALIMA LUBASHA- SERENGETI
ASKARI wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENSPA) kituo cha Tabora B wilayani Serengeti mkoani Mara, Deus Mwakajegera (35) amekatwa mkono wake wa kushoto na jangili,baada ya kumkamata akichunga ng’ombe ndani ya hifadhi kutoka Kijiji cha Bisarara.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishina Mwandamizi Msaidizi ,Masana Moshana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5.00 asubuhi wakati askari akiwa doria na wenzake watatu.
Kamishna Moshana alisema amesikitishwa na tukio hilo kwa sababu askari alikuwa anatekeleza wajibu wake kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa.
Alisema watu wachache wasiozingatia sheria waliamua kuwashambulia askari wao pasipo na sababu za msingi.
Jangili huyo, Zakaria Omahe(54) mkazi wa Kijiji cha Bisarara,baada kufanya ukatili huo alikimbia na kwenda kusikojulikana ambapo uongozi wa kijiji unamsaka.
Alisema Mwakajegera alikuwa doria na askari wenzake watatu ndani ya hifadhi ndipo walimkuta Omahe akiwa anachunga mifugo yake ndani ya hifadhi, huku askari wenzake wakiwa umbali wa mita mia moja hivi wakidhibiti ng’ombe hao wakati anaendelea kumhoji alichomoa panga na kumkata mkono.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bisarara,Mang’era Magesa,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea Kitongoji cha Kinato.
Alisema baada ya askari wenzake kuona mwenzao amekatwa mkoano walikwenda kutoa msaada wa huduma ya kwanza kwa kuufunga ili kuzuia damu isivuje zaidi kwa kutumia magari ya watalii yaliyo kuwa yanapita eneo hilo na kumpeleka Hospitali ya Nyerere DDH kwa matibabu zaidi. Habari kutoka Hospitali ya DDH,zinasema Mwakajegera amehamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi.