20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yaombwa kusaidia wenye ulemavu kuabudu

Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

JAMII imeombwa kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuweka wakalimani katika nyumba za ibada ili nao waweze kushiriki ibada kama wengine.

Akizungumza kwenye mafunzo kwa wanahabari Dar es Salaam juzi, wakati akichangia mada kuhusu changamoto wazipatazo watu wenye ulemavu, Ofisa Utawala Idara ya Ushawishi na Utetezi kutoka Hospitali ya CCBRT, Anna Gugu alisema ukosefu wa wakalimani katika nyumba hizo umekuwa ukichangia watu wengi wenye ulemavu kushindwa kwenda kanisani au msikitini.

Alisema wakati sasa umefika kwa jamii kuona umuhimu wa wakalimani katika maeneo muhimu ili watu wenye ulemavu nao wapate haki zao za msingi.

“Imekuwa jambo la kawaida kushindwa kwenda kanisani kwa sababu kila ninapoenda najikuta sielewi kinachoendelea jambo ambalo limekuwa likinitesa mno kwani natamani kusali,” alisema Anna.

Anna ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa kutosikia, aliwaomba viongozi wa dini kuweka wakalimani ili nao wapate haki hiyo ya msingi ya kuabudu.

Kwa upande wake, Meneja wa Kitengo Cha Ushawishi  a Utetezi wa CCBRT, Fredrick Msigallah, alisema mbali ya uwepo wa sheria zinazowaongoza watu wenye  ulemavu lakini jamii bado haina uelewa kuhusu sheria hizo.

Alisema jamii imekuwa ikiwachukulia watu wenye ulemavu kama ni wasioweza kufanya shughuli yeyote jambo ambalo limekuwa likisababisha wengi kukosa haki zao za msingi ikiwamo kupata ajira halali ili waweze kujipatia kipato.

Msigalla alisema ifike wakati kundi hilo likapewa nyenzo mbalimbali za kufanyakazi ili waweze kujitegemea wenyewe badala ya kuwafanya wawe ombaomba.

Alisema Serikali na wadau mbalimbali wanapojenga nyumba au ofisi zao wahakikishe wanakumbuka kujenga miundombinu ya watu wenye ulemavu ili kuwapa urahisi wa kufika na kupata huduma mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles