22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

MC Pilipili apandishwa kizimbani

Na KULWA MZEE

DAR ES SALAAM

MSHEREHESHAJI Emmanuel Mathias (34), maarufu MC Pilipili na mwenzake, Heriel Clemence (25), wamefikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuchapisha maudhui kwenye mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka  ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Costastine Kakula, akisaidiana na Batrida Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.

Kakula alidai washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui bila kuwa na leseni. MC Pilipili ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach na Clemence Mkazi wa Kawe, wanatuhumiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba 17, 2013 na Mei 2, 2019 katika maeneo tofauti tofauti ndani ya jijii la Dar es Salaam, kupitia televisheni ya mtandaoni inayojulikana kama Pilipili TV .

Washtakiwa walikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo Kakula alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambore, aliomba Mahakama itoe masharti nafuu ya dhamana kwa wateja wake, kwa sababu shtaka linalowakabili linadhaminika.

Hakimu Mmbando alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana, kila mmoja anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua halali za utambulisho na vitambulisho halali ambao watasaini bondi ya sh milioni tano kwa kila mmoja.

Hata hivyo, MC Pilipili alikamilisha masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo Clemence alishindwa kukamilisha kutokana na nyaraka za wadhamini wake kutokamilika. Kesi itakuja leo kwa ajili ya kukamilisha masharti hayo. Kesi itatajwa Juni 4 mwaka huu.

Wakati huohuo, Julius Warioba (23) maarufu kama MC Warioba, naye amefikishwa katika mahakama hiyo kujibu shitaka la kuchapisha maudhi katika Mtandao bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Warioba, ambaye ni mkazi wa Ubungo, wamesomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega.

Wakili wa Serikali, Batilda Mushi, akisaidia na Constantine Kakula, amedai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2016 na Aprili 30, 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la  Dar es Salaam.

Mushi alidai katika kipindi hicho,  Warioba anadaiwa kuchapisha maudhi kupitia Televisheni ya mtandaoni  (Tv online) inayojulikana kwa jina Mc Warioba, bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), wakati wakijua kuwa ni kinyume cha Sheria ya Mtandao.

Mshtakiwa alikana shtaka linalomkabili na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Wakili wa Utetezi, Jebra Kambole, aliiomba mahakama itoe dhamana kwa mshtakiwa huyo, kwani shtaka linalomkabili Warioba linadhaminika.

Hakimu Mtega alitoa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata na barua hiyo ipitishwe kwa Mkurugenzi wa Manispaa, anakotokea mdhamini huyo.

Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles