Na Sheila Katikula, Mwanza Â
Kuelekea sikukuu ya Mwaka Mpya 2021, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ametoa wito kwa watanzania kila mmoa kwa nafasi yake kuwakumbuka watoto yatima kwa kuwapatia misaada mbalimbali ili kuwafanya wajione ni sehemu ya jamii.
Sheikh Kabeke alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea utaratibu wa ofisi yake kuandaa chakula cha pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo mbalimbali jijini hapa kwenye sherehe za mwaka mpya.
Alisema katika sherehe kama hizi ni jambo jema iwapo watu wenye uwezo wataendelea kuwalea na kuwasaidia watoto yatima kwa wema na heri kama vitabu vya mwenyezi Mungu vinavyosema na kama Mtume Muhammad (S.A.W) anavyofundisha kuwa wanaolea watoto hao watapata rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Sheikh huyo alisema kwa kutambua hilo katika sherehe za mwaka mpya mwaka huu ofisi yake imeandaa chakula kwa makundi mbalimbali ya watoto yatima, utaratibu ambao ni muendelezo wa utamaduni ambao ofisi yake iliuanzisha tangu mwaka 2018 alipoingia madarakani na utaendelea kufanyika katika kila sherehe za mwaka mpya kulenga kuwafanya watoto hao kujiona wana thamani kubwa kwenye jamii.
“Naomba nitoe uvumi, kuna watu wanasema huu siyo mwaka wa Waislamu, ni kweli tuna kalenda yetu, lakini huu ni mwaka wetu pia kwa sababu unanza toka alipozaliwa nabii Issa, na sisi tunamtambua kwani vitabu vinasema ili uwe mwislamu hutakiwi kumubagua mtume hata mmoja.
“Tunaamini kuna mitume 25 wametajwa kwenye vitabu na Nabii Issa yupo na vile vile serikali yetu siyo ya kidini hivyo nawaomba watu waondoe fikra mbaya huu ni mwaka mpya wa watu wote ndiyo maana tumeandaa chakula kwa watoto yatima kama fadhira yetu,” alisema Sheikh Kabeke.Â