NA SAMWEL MWANGA -SIMIYU
JAMII imetakiwa kuendelea kutumia mbinu zilizotumika kupambana na ugonjwa wa Covid-19 kujikinga na magonjwa mengine ya mlipuko.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Hamis Kulemba wakati akizungumza na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi jana.
Dk. Kumbela alisema licha ya maambukizi ya ugonjwa huo kuwa chini hapa nchini, ni vyema wananchi wakaendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, iwe sehemu ya maisha yao.
Alisema tahadhari zilizotumika kujikinga na corona, zinapaswa kuwa endelevu kwa vile zinasaidia kujikinga na magonjwa mengine ya mlipuko katika jamii, ikiwamo kipindupindu.
Dk. Kumbela alisema katika kupambana na corona, Watanzania walisisitizwa usafi, kunawa mikono kwa maji na sabuni wakati wote.
“Katika mapambano ya ugonjwa wa corona tulisisitiza usafi, na kila sehemu watu tulinawa mikono kwa sabuni kwa maji yanayotiririka, tahadhari hii tuendelee nayo na tuifanye iwe tabia, ni hakika hatuwezi kupata magonjwa ya mlipuko,” alisema Dk. Kumbela.
Pia alitoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kujilinda kwa vile kazi yao inawakutanisha na watu wengi wa aina mbalimbali, hivyo njia pekee ya kubaki salama ni kufuata taratibu zililozowekwa na wataalamu wa afya kabla na baada ya mikusanyiko.
Alisema kwa mazingira ya kazi yao, waandishi wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuzingatia miongozo hiyo ili kutimiza majukumu yao huku nao wakibaki salama na familia zao.
“Tujitahidi kuendelea kunawa mikono au kutumia vitakasa mikono (sanitizer) mara kwa mara, tunashikana mikono na watu wengi na wa aina mbalimbali kwa siku, pia hata kuvaa barakoa ikibidi, hii itatusaidia kujiepusha na maambukizi ya magonjwa ya mlipuko,” alisema Dk. Kumbela.
Aliwataka kutumia kalamu zao kuelimisha jamii kuendelea kuchukua tahadhari katika kuendelea kukabiliana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Ofisa Habari Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Sara Kibonde, alisema kama jamii itaendelea kufanya yale yaliyofanywa katika mapambano dhidi ya corona, ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, Tanzania itafanikiwa kutokomeza magonjwa ya mlipuko yakiwemo yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
Sara aliwataka waandishi wa habari kutotumia maneno ambayo yataongeza hofu katika jamii wakati wa kuripoti habari za maginjwa ya milipuko.