25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yagawa vyandarua milioni 47

NA FRANCIS GODWIN – IRINGA

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zimesambaza vyandarua  milioni 47 kwa wananchi.

Hatua hiyo ni mpango kabambe wa Serikali kuendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Kazi ya kusambaza vyandarua hivyo bure inaendelea mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya Ofisi ya Rais – Tamisemi, Rashid Maftah, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa kuhusu kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo.

Alisema Serikali imeendelea na kampeni hiyo kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo.

Hadi sasa vyandarua milioni 47 vimetolewa  bure mikoa mbalimbali ili kuwezesha  wananchi kujikinga na mbu.

“Tumeendelea kugawa vyandarua hivi ili  kuikinga jamii na ugonjwa huu hatari wa malaria.

“Natoa wito kwa jamii kutumia vyandarua  kwa malengo yaliyokusudiwa, badala ya  kuvigeuza nyavu za kuvulia samaki ama uzio  wa kuzuia kuku na ndege wengine kuharibu bustani zao za mbogamboga, haya si malengo ya Serikali,” alisema Maftah.

Alisema awali kulikuwa na malalamiko mengi  kuhusu vyandarua vinavyotolewa kuwa ni vidogo havitoshi kwenye vitanda vya baadhi ya wananchi, sasa malalamiko yamefanyiwa kazi na kuleta vyandarua ambavyo ni vikubwa.

Maftah alisema ugawaji umehusisha awamu tatu hadi sasa, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha mikoa ya Rukwa, Mbeya na Songwe na awamu ya pili itahusisha mikoa ya Iringa, Singida na Dodoma.

Aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha  ili kuweza kunufaika na mpango huo wa  Serikali wa ugawaji wa vyandarua vya bure na kampeni hiyo imeonyesha mafanikio makubwa zaidi kutokana na wanaohusika na ugawaji huo kuwa na watumishi wa Serikali.

Naibu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Malaria, Dk. Samwel Nhiga alisema   ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, kwa  sasa kiwango cha ugonjwa huo kimeendelea  kupungua kwa kasi kati ya mkoa na mkoa.

Alisema ili kuendelea kupambana na ugonjwa huo, wamegawa mikoa na maeneo ya nchi kwenye makundi matano na kila eneo limewekewa aina ya afua zinazofaa ambapo  kuna mikoa 10 inagawiwa vyandarua na mikoa mingine haipewi.

Aliitaja mikoa ambayo ina kiwango cha chini cha malaria kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Iringa na Njombe.

“Tutakuja kutoa taarifa rasmi ila kwa sasa  tunataka mjue kuwa Serikali imepambana katika mikoa hii hadi ugonjwa wa malaria kupungua kabisa japo lengo ni kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo 2030, sasa  kufikia huko ni hatua na kuna hatua za  kufanya,” alisema Dk. Nhiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles