27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

JAMII IFUNDISHWE KUYATAMBUA MABOMU

FEBRUARI 24, mwaka huu, watoto wawili wakiwa wanachanja kuni  katika msitu wa Kanyala wilayani Geita walilipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono baada ya kulishika na kuanza kuligonga gonga kwenye jiwe.

Bomu hilo ambalo linasadikika lilibaki katika msitu huo wakati askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakifanya mazoezi,  liliwajeruhi watoto Yohana Alex (18) na Frank Salim (14).

 Watoto kulipukiwa na mabomu hasa yale ya kutupa kwa mikono ni mwendelezo wa matukio hapa nchini kwani mwaka 2012 katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, watoto watano wakati wakiokota vyuma chakavu kwa ajili ya kuviuza kwa wafanyabiashara, walipoteza maisha baada ya  mtoto  Evadius Robert (17) kuliokota bomu  akidhani nalo ni chuma chakavu.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Polisi mkoani Kagera wakati huo, Philip Kalangi alisema, watoto waliopoteza uhai katika tukio hilo ni Evadius Fenias Frank (3), Faraji Frank (1), Edgar Gidion (15), Faustin Alfonce (17) na Patrick Kamali (12).

Si hao tu bali hata miaka kati ya 1991 na 1994 wakati mauaji ya halaiki yamepamba moto nchini Rwanda ambapo wakimbizi walikuwa wakimiminika  mkoani Kagera, watoto si chini ya wawili walipoteza maisha katika Shule ya Msingi ya Tumaini iliyoko  mjini Bukoba baada ya kuokota bomu na kuanza kulichezea wakidhani ni tenesi.

Hayo yakiwa ni matukio machache kati ya mengi ambayo yamewahi kutokea hapa nchini, ni dhahiri vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hususani JWTZ havina budi kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutambua mabomu pamoja na kujikinga dhidi yake.

Vyombo hivi  ambavyo vimepewa jukumu la kuwalinda wananchi, vitakuwa  havijatenda haki endapo vitashindwa kuwaelekeza wananchi kuzifahamu kwa kina baadhi ya silaha hatari za kivita ambazo hubebeka kirahisi na kwa uficho mfano mabomu.

Kwanini kuna umuhimu wa kuwafundisha raia wa kawaida kuhusu utambuzi wa mabomu? Jibu ni kwamba kihistoria kutokana na utulivu wa kisiasa uliopo hapa nchini Watanzania hawana migogoro ambayo inaweza kusababisha vita na hatimaye silaha kutoka mikononi mwa askari na kuangukia kwa raia na hivyo kuzoeleka kama ilivyo Burundi na Somalia.

Pamoja na kutokuwapo vita hapa nchini lakini ikumbukwe kuwa Tanzania siyo kisiwa kwani imepakana na nchi zenye migogoro mfano Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo watu wake wanaweza kuingiza  silaha nchini kwetu kwa njia za panya.

Si tu migogoro ya jirani zetu inaweza kuingiza silaha za hatari hapa nchini, bali pia matukio ya kigaidi yanayoendelea kuitikisa dunia yanaweza kutuletea zahama. Tukio la kushambuliwa kwa ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998 lilikuwa fundisho kwetu.

Mbali na matukio ya silaha kutoka kwa jirani au magaidi lakini pia kuna matukio ya ndani  yasiyokusudiwa yanayoweza kuwa tishio katika  usalama wetu kama ilivyotokea  Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam mwaka 2011  ambapo ghala la zana za kijeshi lililipuka na kuleta taharuki na hivi sasa tumeambiwa bomu lililoleta majanga wilayani Geita ni masalia ya zana za mazoezi ya askari wetu.

Wahenga walisema: ‘‘Kinga ni bora kuliko tiba’’ naamini pamoja na changamoto za  mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ambapo silaha za kisasa zinazidi kuvumbuliwa bado vyombo vya Ulinzi na Usalama vina wajibu kuwaelekeza wananchi kuliko kusubiri mikasa itokee ndipo kuchangamka kuwapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles