MAWAKILI wa Jamhuri katika kesi ya utakatishaji fedha haramu inayomkabili Wakili Median Mwalle na wenzake watatu, wamewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania dhidi ya uamuzi wa Jaji Gadi Mjemas wa kukataa kuvipokea baadhi ya vielelezo vya ushahidi kutoka nchini Marekani.
Vielelezo hivyo viliwasilishwa mahakamni hapo na shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, Suleiman Nyakulinga wiki iliyopita.
Uamuzi huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Jaji Mjemas wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha anayesikiliza kesi hiyo.
Akiwasilisha taarifa hiyo mwishoni mwa wiki mahakamani hapo, Wakili Tibabyakomya aliiomba mahakama hiyo kusitisha kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutokana na kuwasilisha tayari ya kusudio la kukata rufaa.
“Shauri hili haliwezi kuendelea kusikilizwa na kusudio la kukata rufaa limepokewa Desemba 18, mwaka huu kwa ajili ya kupelekwa Mahakama ya Rufaa,” alisema Wakili Tibabyakomya.
Kwa upande wao, mawakili wa utetezi Omary Omary, Innocent Mwanga, Mosses Mahuna, Julieth Tarimo na Emanuel Mvula, walidai mahakamani hapo kuwa rufaa hiyo inawaumiza washtakiwa.
Wakili Omary, alidai kuwa wameshapokea notisi hiyo ya rufaa na kwa kuwa sheria haiwapi nafasi ya kulipinga sualahilo, rekodi inaonyesha hiyo ni namna moja ya kuendelea kuwatesa washtakiwa na kujificha nyuma ya sheria.
“Kwa niaba ya mawakili wa utetezi, tumeshapokea notisi ya rufaa ila hili ni suala ambalo linachukuliwa kwa maumivu makubwa na upande wa washtakiwa, kwani rekodi inaonyesha hii ni namna ya kuendelea kuwatesa washtakiwa kwa kujificha nyuma ya mgongo wa sheria. Hii ni dalili ya wazi ya mawakili wa Jamhuri kupuuza haki za washtakiwa waliokaa gerezani zaidi ya miaka mine,” alidai Wakili Omary.
Kauli hiyo ilimlazimu Wakili Tibabyakomya, kuiomba mahakma hiyo kuweka kwenye rekodi, kuwa hawawatesi washtakiwa hao na kwamba madai ya Wakili Omary, kuwa wanatumia mgongo wa sheria kuwatesa si ya kweli kwani sheria inawaruhusu kukata rufaa pale ambapo hawajakubali uamuzi wa mahakama.
“Malalamiko ya kulenga kuwatesa washtakiwa tunaona hayana msingi wowote kwani hatutumii mgongo wa sheria kuwatesa washtakiwa kwa kuwa sheria inaturuhusu kukata rufaa pale ambapo hatujaridhika na uamuzi wa mahakama,” alidai Wakili Tibabyakomya.
Jaji Mjemas alikubaliana na maombi hayo ya upande wa Jamhuri na kulazimika kuahirisha kesi hiyo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi.
Nyaraka hizo zilizokataliwa na mahakama ni hati saba za viapo, hati mbili za vifo, fomu 13 za mrejesho wa kodi ambazo zilikuwa hazijakidhi matakwa ya sheria ya ushahidi pamoja na sheria inayosimamia upatikanaji wa ushahidi na shahidi nje ya nchi katika makosa ya jinai.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 61 ya mwaka 2015, Wakili Mwalle na wenzake Don Bosco Gichana ambaye ni raia wa Kenya, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi, wanakabiliwa na mashtaka 44 tofauti, yakiwamo ya utakatishaji fedha haramu, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu.