24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Kitwanga aikimbia orodha ya wauza unga

kitwangaNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amepata kigugumizi kuweka hadharani orodha ya majina ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, licha ya kuliagiza Jeshi la Polisi limpatie.

Amesema hata akiwa na orodha hiyo, haitasaidia kukomesha biashara ya dawa za kulevya na badala yake wameunda mfumo utakaosaidia kudhibiti dawa hizo kuingizwa nchini.

Waziri Kitwanga, alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kumalizika kikao chake na maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi Makao Makuu kilicholenga kumpatia taarifa na maelezo ya mambo mbalimbali aliyoagiza, baada ya kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jeshi hilo wiki iliyopita.

“Mtakumbuka hivi karibuni nilitoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kunipatia taarifa za mambo mbalimbali na leo (jana), nimekutana nao, wamenipatia maelezo ya kutosha na tumejadiliana namna watakavyounda mfumo mzuri wa kuhakikisha dawa za kulevya haziingii nchini, na hata zile zilizokamatwa zinateketezwa,” alisema Waziri Kitwanga.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama amepatiwa orodha hiyo alisema: “Kuwa na orodha haiwezi kusaidia, tumejadiliana  namna ya kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa dawa za kulevya.

“Mimi sina ‘list’ (orodha) na sijui kama Rais anayo, nashangaa nyie (waandishi wa habari) mnaandika tu na hata ningekuwa nayo haisaidii kitu maana hatuwezi kwenda kumkamata mtu na kumshtaki bila kuwa na ushahidi.”

Itakumbukwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika utawala wake, aliwahi kuuambia umma wa Tanzania kuwa ana orodha ya wauza dawa za kulevya wakubwa.

Hadi anaondoka madarakani Novemba 5, mwaka huu, hakuwahi kuwataja kwa majina wahusika wakuu wa biashara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Kitwanga alisema mfumo wa sasa wa kudhibiti biashara hiyo hautajali hadhi ya mtu, na kwamba atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kama watu wengine.

“Mfumo hautajali ni mkubwa, mdogo, mwembamba au mnene, atakayekamatwa anachukuliwa hatua mara moja bila kujali cheo chake,” alisema Kitwanga.

Alisema mfumo huo pia umelenga kuzuia vitendo vya kigaidi na wizi katika bandari nchini.

Alisema kikao hicho pia kilizungumzia suala la ubambikaji wa kesi kwa wananchi, ambapo watahakikisha kabla ya mashtaka mtu aliyekamatwa anashtakiwa kwa kosa alilokamatwa nalo ni si vinginevyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, amekanusha taarifa zilizosambaa kuwa jeshi hilo limewasimamisha kazi askari 300, baada ya kubainika kughushi vyeti kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Taarifa hizi hazina ukweli wowote, tunategemea mtu aliyesambaza atasakwa na atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” alisema IGP Mangu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles