LONDON, ENGLAND
NAHODHA wa timu ya rugby ya Harlequins nchini England, James Horwill, juzi alivunjika kidole katika mchezo wa fainali dhidi ya Leicester Tigers, kwenye uwanja wa Welford Road.
Mchezaji huyo alivunjika kidole cha mkono wa kushoto, huku zikiwa zimebakia dakika 10 mchezo huo kumalizika, huku timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 25-6.
Nahodha huyo alionekana kutoa mchango mkubwa kwa timu yake, lakini mchango wake ulikuwa hautoshi hadi anapata tatizo la kuvunjika kidole na nafasi yake ilichukuliwa na Charlie Mulchrone katika dakika ya 70.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, aliwashukuru mashabiki wa timu hiyo kwa kuonesha ushirikiano, japokuwa timu yao ilikuwa nyuma kwa matokeo.
“Nawashukuru wote kwa mchango wao ambao waliuonesha tangu tunaanza hadi mwisho, nasikitika kwamba nimevunjika kidole huku nikiwa napambana kwa ajili ya timu, lakini ninaamini nitarudi tena uwanjani baada ya kidole changu kuwa sawa,” aliandika Horwill.