23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA SASA YAAMUA KUSEMA UKWELI

*Yapanga utambulisho rasmi wa Lwandamina na Pluijm

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


 

b9

HATIMAYE uongozi wa Yanga baada ya kukana kwa muda mrefu taarifa kuhusu kocha George Lwandamina,  umeamua kuweka mambo hadharani kuwa kocha huyo ni wa Jangwani na wanaandaa mipango ya utambulisho rasmi wa Mzambia huyo ambaye atakuwa Kocha Mkuu akirithi mikoba ya  Hans van Pluijm, ambaye atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gazeti dada la MTANZANIA, BINGWA ndilo lilikuwa la kwanza kutoa taarifa hizi kwa uhakika, lakini uongozi wa klabu hiyo kwa matakwa yao walikana taarifa hizo vikali wakiwataka mashabiki, wapenzi wa soka na wale wa Yanga kupuuza taarifa hizo.

Lakini BINGWA na MTANZANIA kwa kuwa walikuwa na imani na chanzo chao cha habari, liliendelea kuandika ukweli mpaka kocha huyo aliyeipeleka klabu yake ya zamani Zesco katika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alipotua na kumalizana nao.

Uamuzi huo wa kukana stori hizo za ukweli inadaiwa ulikuja, baada ya  uongozi huo kutaka kuweka mambo sawa kwa kufanya maboresho katika benchi la ufundi la timu hiyo ambapo kwa sasa yamefikia tamati.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, alisema uongozi huo mpya unatarajia kutambulishwa  rasmi hivi karibuni  kwa wanachama, wapenzi na wadau wa soka nchini.

“Ni kweli tumeingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United nchini Zambia na ataanza kuinoa timu yetu mzunguko wa pili wa ligi,” alisema Sanga.

Akizungumzia kuhusu hatima ya kocha Hans van Pluijm, alisema ataendelea kuwapo kama Mkurugenzi wa benchi la ufundi la timu hiyo.

“Pluijm bado tutaendelea kuwa naye kama Mkurugenzi wa Ufundi kwani ni kocha mzoefu na anaijua vema Yanga, hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kiujumla.

Hata hivyo, Sanga alifafanua zaidi kwamba mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha wao wa awali Pluijm kilikuwa kibaya, bali ni hatua ya uongozi katika kuboresha klabu hiyo ili kuleta changamoto mpya na kujiweka vema katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo.

Sanga alizungumzia hatima ya Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, akieleza kuwa bado wanaitambua nafasi yake hadi yatakapotokea mabadiliko.

“Mara nyingine kocha mkuu ndio anaamua au kupendekeza msaidizi wake si klabu, hivyo bado Mwambusi ni kocha wetu  mpaka hapo itakapotangazwa tofauti, klabu kwa sasa imejikita kwa wakubwa hao wawili,” alisema Sanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles