26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Werema ajiuzulu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam,mtanzaniadaily.2indd
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye ni mmoja wa watuhumiwa katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ametangaza kujiuzulu.
Hatua hiyo ya Werema imekuja wakati Watanzania wakiwa bado wanasubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuhuau maamizio manane ya Bunge yaliyotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyekagua miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika maazimio ya Bunge, baadhi ya viongozi ambao chombo hicho kiliona wana makosa na kutaka mamlaka zao za uteuzi ziwachukulie hatua, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaujuka, Jaji Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa ya TANESCO.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema kutokana na uamuzi wa Jaji Werema, Rais Kikwete amekubali ombi la kujizulu kwa mwanasheria mkuu huyo.
Ilisema katika barua yake, Jaji Werema amesema ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.
“Kuanzia leo (jana), Desemba 16, 2014 na Rais Jakaya Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Jaji Werema na amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu
Wabunge wafunguka
Zitto amshangaa Jaji Werema
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema ameshangazwa na sababu ambazo Werema amezitoa katika barua yake ya kujiuzulu.
“Alipaswa kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa uzembe wa matumizi mabaya ya ofisi. Hata Rais Kikwete asipofanya hivyo, rais ajaye atafanya hivyo,” alisema Zitto.
Kafulila: Afikishwe mahakamani
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye ndiye aliyeifikisha kashfa hiyo bungeni kwa mara ya kwanza, alisema kujiuzulu kwa Jaji Werema pekee haitoshi bali wote waliotajwa na Bunge wanapaswa kujiuzulu au kufukuzwa kazi, kurudisha fedha zote zilizochotwa na kufikishwa mahakamani kwa kuhujumu uchumi.
“Kwanza alichelewa kuchukua uamuzi huo na kuchelewa kwake na kwa wengine ambao bado wapo kimya ni kwa sababu wanajua wakubwa wanahusika na wanamtega Rais.
Mramba (Basil Mramba, aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha) alisamehe Sh bilioni 11 za kodi hivi sasa yuko mahakamani, iweje hawa waliosababishwa kuchotwa Sh bilioni 321, kufanya wahisani wakate misaada ya zaidi ya Sh bilioni 900 na kuchafua nchi kimataifa waishie kujiuzulu tu?” alihoji na kuongeza:.
“Wakati wa mkutano wa Bunge, Spika (Anne Makinda) alisema viongozi wengine waliokuwa na tuhuma walikuwa wanajiuzulu wenyewe lakini hawa waligoma, hawa walikuwa wanafanya hivyo kwa sababu wanamtega rais,” alisema Kafulila.
Sendeka
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema hatua ya kujiuzulu Jaji Werema pekee haitoshi ila sheria ichukue mkondo wake kwa watu wote walioliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Alichelewa kufanya hivyo na hii haitoshi kwa Jaji Werema pekee kujiuzulu ila hatua za sheria zichukuliwe kwa watu wote waliotajwa ikiwamo kwa Rais Kikwete kuwawajibisha n wote waliotajwa katika kashfa hii na kubainika kama Bunge lilivyopendekeza,” alisema Sendeka.
SPIKA MAKINDA
Novemba 28 mwaka huu, Spika Makinda alisema uamuzi wa kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, umekuwa mgumu kutokana na viongozi hao kugoma kufanya hivyo.
“Suala hilo limekuwa tofauti kwa sababu wale wa mwanzo walijiuzulu wenyewe lakini hawa hawataki, je tunafanya nini? …. ndiyo maana hapa tunaandaa maazimio,” alisema.
Maazimio ya Bunge
Novemba 29, mwaka huu Bunge lilipitisha maazimio manane baada ya maridhiano kati ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kambi ya Upinzani, upande wa wabunge wa chama tawala CCM na Serikali.
Baadhi ya maazimio hayo ni lile lililosema: “Kwa kuwa Taarifa Maalum ya Kamati imeonyesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya fedha ya shirika hilo;
Kwa kuwa ,Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo,”.
Pia lilipitisha azimio la kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni Victor Mwambalaswa (Kamati ya Nishati na Madini), William Ngeleja (Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti).
Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na mgao wa fedha hizo ambapo Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa Serikali alipewa mgawo wa Sh bilioni 1.6 huku Ngeleja akipewa Sh milioni 40.2.
Balozi awa mbogo
Desemba 12 mwaka huu, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, alisema ni lazima ahadi hizo zitekelezwe kabla Marekani haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania.
“Tunafurahi kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania.
“Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini Tanzania. Tumetiwa moyo na tamko lililotolewa na Ikulu Desemba 9 kwamba hivi karibuni litashughulikia maazimio ya Bunge kuhusu IPTL.
“…tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo,” alisema Balozi Childress
Alisema katika mkutano huo bodi iligusia makubaliano kadhaa yaliyofanyika ambako Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya sera, muundo na taasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake na katika sekta ya nishati kwa upana wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles