Na Elizabeth Hombo, aliyekuwa Arusha
JAJI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustine Ramadhan amesema suala la mgogoro wa Zanzibar linamuumiza rohoni na kumyima raha.
Kutokana na hilo, amesema hivi sasa suala hilo ameliweka katika maombi maalumu ya kila siku ili haki itendeke na walio katika ngazi za uamuzi waamue kwa haki.
Jaji huyo ambaye ni miongoni mwa watu wanaoheshimika ndani na nje ya Tanzania, ametoa kauli hiyo ikiwa imepita zaidi ya miezi mitatu sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Uchaguzi huo uliofutwa na Jecha Oktoba 28 mwaka jana kwa kile alichodai kuwepo kasoro mbalimbali, tayari wiki chache zilizopita alitangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi huo kuwa ni Machi 20 mwaka huu.
Jaji Ramadhani ambaye hivi sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika ofisini kwake jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
“Hilo ningeomba nisiliseme…lolote nitakalolisema linaweza kuongeza mafuta kwenye moto mpaka dakika hii wewe unajua wamezungumzia watu mbalimbali mara huyu kasema hivi mwingine vile.
“Hivyo nisingependa kusema maoni yangu hadharani, nilikuwa tayari maoni au msaada wangu niutoe kwa wahusika lakini sikushirikishwa na wahusika.
“Tangu hapo nimekuwa nikilisalia ninaombea amani Zanzibar kwa sababu ni kwetu kule kuna ndugu zangu, makaburi ya wazee wangu hivyo linanihusu na kila ninapotoa misa ninaombea,”alisema.
Jaji Ramadhani ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa Kuu la Anglikana Zanzibar, alisema ameamua kufanya maombi hayo kwa kuwa anaumizwa na mgogoro huo wa Zanzibar.
“Babu yangu ambaye mwenye jina ninalolitumia la Ramadhan ni mwanzilishi na wa chama cha Shirazi Association ikabadilishwa ikawa Afro Shirazi (ASP)hivyo Personally ninaumia kwa kazi ambayo babu yangu alianzisha.
“Ninachokifanya kwa sasa ninamwomba Mungu hao wenye maamuzi waweze kuona na kufanya maamuzi yaliyo sahihi na kihaki, usalama na amani idumishwe kwa sababu Mungu wetu ni wa haki hivyo ninaomba awasimamie.
“Ningeomba amani kule idumishwe kama ilivyo huku bara. Wewe unakumbuka mimi nilikuwa mmoja wa wagombea wa urais ndani ya CCM lakini sikupata nafasi hata ya kucheketwa kwenye vikao lakini kwa kutumia kalamu tu nikafutwa pamoja na wengine chungu nzima lakini nilikaa kimya hivyo hata kwa Zanzibar busara kama hizi zitumike,”alisema jaji huyo.
Pamoja na hilo alishauri kuwa mgogoro huo umalizwe kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu hata uhuru wa Tanganyika ulipatikana kwa namna hiyo.
“Pamoja na kwamba kuna mazungumzo yaliyofanyika, waendelee kuzungumza kwa sababu hakuna jambo linaloshindikana kwenye meza…hata uhuru wa Tanganyika tuliupata kwenye meza ya mazungumzo,”alisema Jaji Ramadhani.
KUHUSU HIZBU
Akizungumzia kuibuka vitendo vya ubaguzi yakiwamo mabango katika sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jaji Ramadhani alishangazwa na hali hiyo.
Alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM kubeba bango lililokuwa likiashiria ubaguzi wa rangi wakati wa sherehe hizo ni hali inayosikitisha kwa mustakabali wa taifa letu.
“Binafsi limenisikitisha sana kwa sababu kule kuna wazee wangu, kama nilivyokwambia kuwa babu yangu ni mwanzilishi wa Shirazi Association hivyo nikiona vitendo vya ubaguzi kama vile ninaumia…lakini nilimsikia baada ya pale kiongozi mmoja wa CCM aliomba radhi.
“Hivyo ni vyema kukawa na maelewano kama huku bara baada ya uchaguzi kulitulia watu waliweka tofauti zao pembeni.
“Inasikitisha sana. Hivi mimi wazazi wangu ni chotara, wakanizaa hivi nilivyo sasa mtu anaponihukumu kosa langu liko wapi? Mungu kaniumba hivi. Hii ni sawa na mtu kujilaumu juu ya jinsia yake kwamba kwanini nimeumbwa mwanamume au mwanamke…hivyo ubaguzi wa aina yoyote ni mbaya, lazima ukemewe,”alisema.