24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi MSD atumbuliwa jipu akipanga vitanda Muhimbili

ummy mwalimuCHRISTINA GAULUHANGA NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

MACHUNGU ya utumbuaji majipu kwa viongozi  na watendaji wa Serikali  yameshiuka kasi ambapo  katika hali ya kuhuzunisha Mkurugenzi wa Manunuzi wa Bohari Kuu la Dawa (MSD),  Herry Mchunga, amejikuta akitumbuliwa wakati akiendelea na ufungaji wa vitanda vipya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Tangu juzi Mchunga, alikuwa kihaha kuhakikisha anatimiza majukumu hayo baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli, ambaye alitoa siku 30 kuhakikisha wanafunga vitanda katika wodi ya wazazi pamoja na kupeleka vifaa tiba.

Wakati akiendelea na shughuli hiyo hospitalini hapo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ghafla alibadili upepo na kutangaza kusimamishwa kazi kwa watendaji wa MSD akiwemo Mchunga

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Waziri Ummy, alimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya MSD, Profesa Idrisa Mtulya,  kuwasimamisha kazi watendaji hao kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha na kukiuyka sheria ya utumishi wa umma.

Pamoja na kutolewa kwa maagizo hayo, wakati wote Mchunga  alikuwa haelewi kinachoendea  huku akiwa anaenaelekea katika tukio la kukabidhi vifaa tiba, alijikuta akizuiwa na wafanyakazi wenzake wa MSD na kwenda naye pembeni na kumuarifu uamuzi wa Waziri Ummy wa kumsimamisha kazi.

Kutokana na tukio hilo watumishi hao walimchukua Mchunga na kwenda naye kwenye gari na kumtaka aondoke katika eneo hilo huku wananchi na wanahabari wakiwa wamepigwa na butwaa.

Baadhi ya watendaji wa MSD na wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, walisikika wakisema hatua ya kufika kwa vifaa  katika hospitali hiyo imetokana na nguvu kubwa aliyokuwa akiitumia Mchunga ambaye kila wakati alikuwa akihangaika kuhakikisha agizo la Rais Magufuli, linatekelezwa kwa wakati.

“Aisee roho imeuma sana…wote tumepoteza nguvu ya kufanyakazi kwani Mchunga ndiye alikuwa kinara wa shughuli ya leo (jana), tunaweza kusema kufika kwa vifaa hivi yeye ndiye aliyekuwa na mchango mkubwa tunaomba uchunguzi wa haki ufanyike ili kila mtu apate haki yake,” alisikika mmoja wa wafanyakazi hao akisema.

Baada ya muda mfupi kupata taarifa Mchunga aliondoka katika viwanja hivyo na kuacha shughuli za kukabidhi vifaa hivyo zikiendelea.

Hata hivyo baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti walionekana kukosoa utumbuaji majipu wa aina hiyo na kudai kuwa unaweza kuhatarisha maisha ya wahusika au watuhumiwa.

“ Du utumbuaji wa aina hii ni balaa ni vyema ikatafutwa namna nyingine kwani mtu yupo kazini anaendelea na kazi halafu anasimamishwa kazi ghafla inauma sana,”alisema mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Agizo la Waziri

Pamoja na kuondoka kwa Mchunga katika eneo hilo, Waziri Mchunga, aliagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi wanne wa MSD .

Alisema kutokana na ubadhilifu wa fedha Sh bilioni 1.5 ndani ya MSD tayari uchunguzi wa ndani ulikwisha kamilika na kinachosubiriwa ni hatua za mwisho ili kujiridhisha kama wakurugenzi hao wanahusika kwa namna moja ama nyingine.

“ Namuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya MSD, Profesa Idrisa Mtulya, kuwaandikia hii leo (jana) barua wakurugenzi wanne ambao wanatuhumiwa kutumia vibaya fedha za Serikali Shilingi bilioni 1.5 ambazo zilitumika kununuliwa vifaa tiba mbalimbali , hatua hizi zichukuliwe kwa uzito wake kuanzia leo (jana),” alisema Ummy.

Aliwataja wakurugenzi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Manunuzi, Herry Mchunga, Mkurugenzi wa Ugavi, Misanga Muja, Mkurugenzi Shughuli za Kanda ambaye pia alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa MSD kwa miaka mitatu, Cosmas Mwaifwani na Mkurugenzi wa Fedha na Mipango , Joseph Tesha.

Waziri huyo wa Afya, alisema ni vyema Mwenyekiti wa bodi ya MSD, akachukua hatua za haraka kuwaandikia barua watumishi hao ili uchunguzi zaidi wa nje uendelee.

Alisema Serikali ya awamu ya tano haipo tayari kuwafumbia macho watumishi watakaobainika kujihusisha na ubadhilifu wa fedha hususan katika sekta ya afya.

Aliongeza kuwa atahakikisha sekta hiyo inafanya vizuri na hatakuwa tayari kufumbia macho watumishi ambao watakiuka maadili na kumsababishia yeye kufukuzwa kazi au kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Agizo hilo limetekelezwa baada ya Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Watoto, Dk.Khamis Kigwangwala kutoa agizo Januari 30, mwaka huu, mjini Arusha wakati wa uzinduzi wa duka la dawa ambapo aliagiza baadhi ya wakurugenzi wa MSD wasimamishwe kazi ndani ya siku 14 kutokana na ubadhilifu wa fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles