21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mutungi asema siku za mwizi arobaini

Jaji Francis Mutungi
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema hana haja ya kuhangaika na tuhuma zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa ofisi yake inatumiwa ili kukisambaratisha chama hicho.

Amewataka Watanzania watulie na ukweli utabainika tu, ikizingatiwa siku za mwizi ni arobaini.

Jaji Mutungi alisema hayo jana, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu tuhuma zilizoelekezwa katika ofisi yake na Chadema.

“Anayesema ofisi yangu inatumika tumwache aseme lakini ‘data na facts’ zitaeleza ukweli… mwizi mpe siku arobaini utambaini. Nasikitika na wanaosema hivyo, lakini katika mpira na siasa haya yapo.

“Sisi bwana ni kama refa, tukiletewa kitu tunashughulikia. Wanachama wanaotaka kujua ukweli watajua tu,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Chadema kumtaka ajitokeze hadharani kubainisha ukweli iwapo yeye ndiye aliyemtuma msaidizi wake, Sisty Nyahoza kusema kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hana sifa ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho kutokana na kuzuiwa na Katiba ya Chadema.

Nyahoza alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema Mbowe hana sifa za kugombea uongozi wa chama hicho, kwa vile katiba ya chama hicho inambana.

Alisema kipengele cha ukomo wa mgombea katika katiba Chadema ya mwaka 2006 kiliondolewa kinyemela bila idhini ya mkutano mkuu.

Nyahoza alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2004 ilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka kilichoeleza kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi viwili vya miaka mitano mitano hawezi kuwania tena nafasi hiyo.

Mvutano huo ulikifanya chama hicho kumlaumu Msajili, Jaji Mutungi, kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.

Julai mosi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama hicho, bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.

Mnyika alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa, bali iliundwa upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13, 2006 ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati huo, John Tendwa.

Alisema katika mchakato huo yalikuwapo mabishano na makubaliano katika baadhi ya masuala, lakini suala la ukomo wa uongozi liliafikiwa na wanachama wote bila tatizo na kupitishwa kuingizwa katika katiba na Ofisi ya Msajili ilipelekewa fomu ya marekebisho na katiba mpya kama sheria inavyotaka.

“Tunachomtaka Mutungi ni kuheshimu katiba ya chama na kuwaheshimu wanachama wa Chadema na ayapuuze madai ya wasaliti wachache. Kama vipi asubiri aone uamuzi wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ubainishe kama katiba ilivunjwa,” alisema Mnyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles