Na KULWA MZEE
-DAR ES SALAAM
Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma amewaonya viongozi wa serikali watakaoingia katika anga zao kwa kuvunja amri za mahakama na kuwataka wabaki katika nafasi zao za kikatiba bila kuingilia uhuru wa mahakama kwani ndiyo yenye mamlaka ya kutoa haki.
Amesema kuanzia sasa watakuwa wanawaita na kuwachukulia hatua kama Bunge linavyofanya na watakuwa wakali endapo watu wataingia katika anga zao.
Jaji Mkuu amesema hayo leo Jumanne Januari 23, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya Sheria itakayoanza Januari 27 na kumalizika Februari Mosi mwaka huu.
“Kuanzia sasa mtu akiingia kwenye anga zetu wakiwamo wale wanaoingilia uhuru wa mahakama, tutafanya kama Bunge linavyofanya, tutawaita na kuwahoji na kujieleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua,” amesema Jaji Profesa Juma.