27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU ATIA NGUMU KWA MAHAKIMU

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM     


MAHAKAMA ya Tanzanja imewataka Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo wenye vyeti vya daktari ambavyo vinawakataza kufanya kazi vijijini, wasisaini mkataba wa kiapo cha kufanya kazi hiyo.

Hayo yalibainishwa jana na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Profesa Ibrahimu Juma, alipokuwa akiwaapisha Mahakimu Wakazi 65 wa Mahakama za Mwanzo.

Jaji Juma alisema kiapo chao kimechukua muda mfupi lakini uzito wa kiapo hicho ni zaidi ya miaka yote waliyosoma na zaidi ya miaka yote watakayokuwa kazini.

“Mahakimu mko karibu na wananchi na maeneo mnayopangiwa pengine mbali na huduma za kijamii, lakini mnatakiwa kufahamu wananchi nao wanastahili kupata huduma.

“Baada ya kiapo wengine watajitokeza na vyeti vya daktari vinasema asifanye kazi vijijini, kama yupo mwenye vyeti asisaini huo mkataba wa kiapo,” alisema na kuongeza kwamba mahakimu wanatakiwa kufanya kazi maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema katika kazi hiyo ya kutoa haki watakutana na changamoto za majengo, miundombinu, wasishtuke wanapoonyeshwa ofisi zao kwani hiyo ndio hali halisi ya Tanzania.

Changamoto nyingine watakayokutana nayo ni weledi kwani wananchi wanahitaji weledi kutoka kwao, wanataka hukumu na nakala za hukumu zipatikane kwa haraka lakini zinazozingatia weledi.

“Kuna changamoto ya sheria, kanuni huenda za zamani hazieleweki, msilalamike bali wajulisheni wakuu wenu wa kazi, kamati itapita na huenda sheria hiyo ikabadilishwa.

“Watanzania hawafahamu haki kwa mujibu wa sheria, wengi wakishinda ndio wanasema haki lakini wakishindwa wanasema hakuna haki, wananchi wanatakiwa kuelimishwa kujua haki zao,” alisema.

Changamoto nyingine ni kushirikiana na wadau wakiwemo polisi, magereza,  wakuu wa mikoa na wilaya.

Alisema lazima wawe na ushirikiano na wadau hao wa mahakama bila mwingiliano katika mipaka ya kazi.

“Eneo jingine lenye changamoto ni rushwa, mahakama haikubali rushwa, kama kuna mtu amekuja kwa ajili ya maslahi nje ya maslahi yaliyomo katika barua yake ya ajira, kazi hii haimfai.

“Haipendezi na ni aibu hakimu kufikishwa mbele ya Hakimu mwenzako kwa rushwa, ukifikishwa mahakamani kwa rushwa hata kama utashinda kesi utastaafishwa kwa maslahi ya umma,” alisema.

Profesa Juma aliwataka mahakimu hao kufuata utaratibu wa kufikisha malalamiko yao na kwamba hawastahili kulalamika lalamika na wakimwona anayelalamika huyo ana matatizo.

Alisema mahakimu ndio wamesambaa nchi nzima, mahakimu wa makahakama za mwanzo wamebeba mashauri asilimia 70, mahakama ya mkoa asilimia 12, Mahakama Kuu na rufaa zina mashauri machache.

“Changamoto ni nyingi mnatakiwa kuharakisha kutoa hukumu na nakala za hukumu zinapatikana bure.

“Mkiletewa malalamiko muyatatue, lazima mjue changamoto za Tanzania kwa ujumla na zile zinazoikabili mahakama, wote mna wazazi. Usimwombe mzazi zaidi ya uwezo wake,” alisema Jaji Profesa Juma.

Miongoni mwa mahakimu wakazi 65 waliokula kiapo jana, mahakimu 17 hawakufika katika hafla ya kuapishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles