27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI: MAHAKAMA ILIINGILIWA

JANETH MUSHI Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA

VILIO, shangwe na nderemo jana vilitawala katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuachiwa huru kwa dhamana.

Mwanasiasa huyo machachari ameachiwa huku akiandika rekodi ya kukaa mahabusu katika Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi minne baada ya kukosa dhamana.

Lema aliachiwa kwa dhamana jana wakati mahakama hiyo ilipokuwa ikisikiliza rufaa ya Jamhuri namba 135 ya mwaka jana, inayopinga uamuzi wa Novemba 11, mwaka jana wa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha wa kumpa Lema haki ya dhamana.

Shangwe zililipuka katika ukumbi huo wa mahakama mara baada ya Jaji Salma Maghimbi wa mahakama hiyo kumwachia Lema kwa masharti ya kujidhamini mwenyewe pamoja na kudhaminiwa na wadhamini wengine wawili ambao kila mmoja alisaini hati yenye thamani ya Sh milioni moja.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Maghimbi alisema mahakama ya chini ilishindwa kusimamia mamlaka yake vizuri hivyo kuingiliwa kabla haijamaliza mwenendo wake.

Jaji huyo alisema mahakama ikitamka dhamana iko wazi inatakiwa kukamilisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na mshtakiwa kudhaminiwa na kama upande wa pili utakata rufaa kupinga ufanye hivyo  baada ya uamuzi kutolewa.

Pamoja na hilo alisema kwa mamlaka iliyonayo Mahakama Kuu ya kuzisimamia mahakama za chini baada ya kubaini tatizo kuanzia mazingira ya kesi hiyo na Lema kukaa gerezani muda mrefu, iliamua kujivika madaraka ya kukamilisha masharti ya dhamana yenyewe.

Jaji Maghimbi alisema Mahakama Kuu imeamua kumalizia kazi iliyopaswa kufanywa na mahakama ya chini na hivyo kutangaza kufuta notisi ya kusudio la kukata rufaa iliyotolewa na mawakili hao Novemba 11, mwaka jana kwa kile alichosema ilikosa mashiko na misingi ya kisheria.

“Nashangaa hakimu aliruhusu vipi mtu asimame wakati wa mwenendo, hivyo nakubaliana na hoja za wajibu rufaa na mahakama ilipaswa kusubiri mpaka mwisho ikague wadhamini na ninakemea mahakama za chini zisimamie madaraka yake kwa sababu isiposimamia madaraka yake vizuri itachezewa na watu hawatapata haki zao,” alisema Jaji huyo.

Katika rufaa hiyo mawakili wa Serikali walikuwa wakipinga mahakama ya chini kumpa Lema dhamana kwa vielelezo kuwa usalama wa mwanasiasa huyo utakuwa hatarini iwapo atakuwa nje.

Lema alikuwa akiwakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongozwa na Peter Kibatala, Adam Jabir, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula wakati Jamhuri iliwakilishwa na Faraja Nchimbi na Paul Kadushi.

 

RUFAA YA LEMA YAONDOLEWA

Baada ya uamuzi huo, mawakili wa Lema waliomba kuondoa mahakamani hapo rufaa namba 126 iliyokatwa na mbunge huyo dhidi ya Jamhuri ambayo ilikuwa inapinga na kudai haki ya dhamana ya kiongozi huyo.

Baada ya rufaa ya Jamhuri kufutwa, huku akilia wakili Kibatala naye aliiomba mahakama hiyo kufuta rufaa ya mteja wake kutokana na kupewa dhamana, ambapo jaji alikubali ombi hilo.

ILIVYOKUWA MAHAKAMA ZA CHINI

Novemba 11, mwaka jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Paul Kadushi, alisimama wakati hakimu huyo akijiandaa kuandika masharti ya dhamana na kuieleza mahakama hiyo kuwa wameshasajili notisi ya kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa hakimu huyo kumpa Lema dhamana.

Hata hivyo, uamuzi huo wa dhamana haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.

Hakimu Kamugisha alishindwa kuendelea na masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo ambapo alikubaliana na upande wa Jamhuri na kusema kuwa notisi ina hadhi sawa na maombi ya rufaa yaliyowasilishwa Mahakama Kuu hivyo mwenendo na uamuzi wake utasimama hadi uamuzi utakapotolewa na Mahakama Kuu.

Januari 4, mwaka huu, Jaji Maghimbi alitarajiwa kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusiana na dhamana ya Lema hata hivyo ilikwama baada ya mawakili wa Serikali kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, kupinga Jaji huyo  kusikiliza rufaa yao wenyewe.

 

MAWAKILI WAOMBA KUWASILISHA HOJA

Awali kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa saa 5:21 asubuhi, Wakili Mkuu wa Serikali, Nchimbi aliiomba mahakama hiyo kuwaongezea muda wa kuwasilisha hoja zao za kuunga mkono rufaa hiyo kwa njia ya maandishi.

Alisema Desemba 28, mwaka jana mahakama hiyo iliagiza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja zao kwa maandishi ila walishindwa kutokana na rufaa waliyokata Mahakama ya Rufaa Tanzania.

“Kufuatia rufaa ya DPP ambayo ililazimisha mwenendo wa shauri hili kusimama, upande wetu tulishindwa kuwasilisha hoja za kuunga mkono rufaa, mahakama ikikubaliana na ombi hili baada ya dakika 15 au muda utakaopangwa na mahakama tutakuwa tumewasilisha hoja zetu,” alisema.

 

Naye Wakili Kibatala alisema hawana pingamizi na ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo kuwapatia muda wa saa moja ili waweze kuwasilisha majibu kwa njia ya maandishi.

Jaji Maghimbi alikubaliana na maombi hayo ambapo aliahirisha kesi hiyo saa 5:30 asubuhi na kuagiza upande wa Serikali kuwasilisha hoja zao saa 11:45 na upande wa wajibu rufaa saa 12:45 na kuahirisha kesi hiyo hadi saa 1:30 mchana.

Wakati Mahakama Kuu ikitoa uamuzi wake huo jana, Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema waliokuwepo mahakamani hapo ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye na Naibu Katibu Mkuu  Chadema Bara, John Mnyika.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salim Mwalimu, Prof. Abdallah Safari, Prof. Mwesiga Baregu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Arcado Ntagazwa, Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, Joseph Mbilinyi ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini, wabunge na viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa na wilaya.

KAULI YA LEMA NJE YA MAHAKAMA

Akizungumza na viongozi, wafuasi na waandishi wa habari nje ya Mahakama hiyo baada ya kuachiwa kwa dhamana, Lema alisema alichopanga kuzungumza hataweza kuzungumza kwa kuwa ameandaa waraka kwa ajili ya Rais Dk. John Magufuli na anatarajia kuutoa hivi karibuni.

Akizungumzia kwa ufupi maisha ya gerezani, Lema alidai kuwa ameona mateso mengi ya watu.

“Nina machache sana ya kuongea, kwanza namshukuru Mungu, Jamhuri ilikusudia mabaya kwangu lakini Mungu amenikusudia mema, vile vile namshukuru sana mke wangu kama ningepata fursa ya kuoa tena ningemuoa yeye, nawashukuru familia, mawakili, viongozi na wengine, nikisema niongee ninachotaka kuongea leo sitaweza,” alisema na kuongeza:

“Nitautoa waraka huo siku za hivi karibuni kwa rais, nimeona mateso mengi ya watu na kwa sababu mara ya mwisho mtoto wangu mdogo wa mwisho aliniuliza akaniambia baba, nifanye kosa gani ili nije nilale na wewe magerezani? Naomba nikamuone kwanza yeye na nikamshukuru kwanza Mungu, asanteni sana, Mungu awabariki wote.”

 

KIBATALA: TUNAJIPANGA

Naye wakili Kibatala alisema baada ya rufaa hiyo kuisha, sasa wanatarajia kujipanga katika kesi ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwani wanaamini wana kazi muhimu ya kuifanya huko kwa uwezo wao wote.

“Leo tunawakabidhi Lema, samahanini safari imekuwa ni ndefu, imechukua muda mrefu lakini kama ambavyo Mahakama Kuu ilivyosema, haikuwa tatizo au kosa letu na imeelekeza mahakama za chini zisimamie madaraka na mamlaka yake bila kuyaachia,” alisema na kuongeza:

“Mteja wetu alituambia hataki kutoka kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kwa namna ambayo itahakikisha mtu mwingine yeyote hatapitia njia hiyo na leo Mahakama imetengua hilo suala kwa hiyo ile hali mtu anapata dhamana unaweka kusudio la kukata rufaa halafu mikono ya mahakama inafungwa limemalizwa rasmi leo.”

 

MBOWE ALAANI POLISI

 

Akizungumza kwa niaba ya chama hicho, Mbowe alilaani vikali hatua ya Jeshi la Polisi kuwapiga wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakitaka kuingia mahakamani hapo jana kusikiliza kesi hiyo.

Mbowe alikiita kitendo hicho kuwa ni cha uonevu ambao alisema watakwenda kuujadili bungeni pamoja na katika majukwaa mbalimbali ili kukomesha.

“Lema anatakiwa aende nyumbani akakae na familia yake na watoto wake, hakutakuwa na tukio lolote la kisiasa siku ya leo na natumia  nafasi hii kulaani Jeshi la Polisi kwa sababu wamepiga sana vijana wa Chadema nje, wamewapiga wapita njia wameonea, kuwaumiza na wengine wamewekwa rumande bila sababu za msingi,” alisema Mbowe na kuongeza:

 

“Huyu ni mbunge wa watu lazima watu wampokee, ila polisi wanapotumia mamlaka yao na silaha zao kuumiza raia hili halikubaliki, nitamtafuta RPC na RCO kwani wajibu wao katika mkoa huu ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na si kuonea raia.”

 

BABA WA LEMA ATOA NENO

 

Naye baba mzazi wa mbunge huyo, Jonathan Lema, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuwa jasiri na wavumilivu.

Akimzungumzia mwanawe, alisema hakuwa na wasiwasi juu ya dhamana yake kwa sababu alitumaini ipo siku ataachiwa kwa dhamana.

Alisema kunyimwa dhamana kwa Lema ilikuwa ni kumpotezea muda tu.

“Leo kwangu naona kama Lema  amezaliwa upya, nawasihi wananchi wasikate tamaa wazidi kusonga mbele, nilikuwa nafika mahakamani nikiwa na furaha na matumaini kuwa atatoka baada ya kuangalia vipengele vya sheria kwani kesi yake ina dhamana, nilijua kesi za ugaidi au mauaji ndiyo mtu hapati dhamana, ila hii ilikuwa kumpotezea muda na nimejifunza uvumilivu,” alisema mzee huyo.

 

Kwa upande wake mke wa Lema, Neema Lema, huku akilia alisema kwa siku ya jana hawezi kuzungumza chochote kuhusu mume wake kupewa dhamana.

Wakati kesi hiyo ikitolewa uamuzi jana katika kila kona ya viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha kulikuwa na ulinzi  mkali wa askari polisi wenye silaha za moto,  mabomu ya machozi, mbwa na gari la maji ya kuwasha.

Kuimarishwa kwa ulinzi huo kulikwenda sambamba na kamata kamata ya watu wengi wao wakiwa ni vijana waliokuwa wamesimama nje ya uzio wa mahakama hiyo.

Mbali na kesi ya Lema, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido, Onesmo Ole Nangole, aliwasilisha maombi ya kukata rufaa mahakamani hapo hatua iliyochangia pia kuwapo kwa watu wengi ndani na nje ya mahakama.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani vya jeshi hilo zilidai kuwa kuwapo kwa viongozi wa Kamati Kuu ya Chadema kulichangia jeshi hilo kumwaga askari wengi kuliko kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles