28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Jaja aanza kuonyesha makali Pemba

Santos Santana ‘Jaja’
Mchezaji wa Yanga Geilson Santos Santana ‘Jaja’ akipokea nakala ya mkataba wake kutoka kwa Katibu Mkuu wa yanga, Beno Njovu, jana baada ya kusaini kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili.

NA HUSSEIN OMARI, PEMBA

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga Mbrazil Geilson Santana ‘Jaja’, jana ameanza kuonyesha makali yake baada ya kuifungia timu yake bao, katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Chipukizi, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Gombani, Chakechake Pemba.

Mchezaji huyo amejiunga na Yanga mwezi mmoja uliopita, akionekana hatakuwa na msaada wowote katika klabu hiyo kutokana na mashabiki kuanza kumbeza kufuatia kupambwa na magazeti.

Jaja aliipatia timu yake bao la ushindi katika dakika ya 6, akipokea krosi safi iliyochongwa vizuri na Haruna Niyonzima na yeye kuimalizia kwa kichwa.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Maximo alisema wachezaji wake wameonyesha uwezo mzuri na amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake, ambapo watajipima zaidi katika mechi za kirafiki dhidi ya Shangani Zanzibar, Jumapili.

“Nimefurahishwa sana na uwezo wa wachezaji wangu, nimeridhika na kile walichokifanya ni imani yangu wataendelea kufanya vizuri katika mechi zinazokuja,” alisema.

Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, Yanga walionekana kuonyesha uwezo mkubwa wa kuweza kuikabili timu hiyo na kufanikiwa kupata bao hilo mapema.

Maximo aliwatumia wachezaji Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Andrey Couthinho, Haruna Niyonzima, Jaja, Mrisho Ngassa na Kelvin Yondani katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Yanga iliwatumia wachezaji Juma Kaseja, Zahir Rajab, Omega Seme, Said Bahanuzi, Hamis Kiiza, Nizar Khalfan, Jerryson Tegete na Salum Telela, ambapo katika kipindi hicho cha pili kikosi hicho kilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini Chipukizi walikuwa makini katika kuhimili mipira.

Kwa nyakati tofauti wachezaji Hamis Kiiza na Tegete walikosa mabao ya wazi, ambapo kila mmoja kwa wakati wake alikosa bao akiwa amebaki yeye na kipa, Maximo aliwatoa na kuwaingiza Hamis Thabit, Amos Abel.

Dhumuni kubwa la Maximo, lilikuwa kuangalia uwezo wa kila mchezaji na kuona wameelewa kwa kiasi gani kile alichokuwa anakifundisha kwa takriban mwezi mmoja sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles