26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jafo apiga marufuku viongozi kuwadhalilisha walimu

Na SHEILA KATIKULA – MWANZA


WAZIRI wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amewataka viongozi nchini kutowadhalilisha walimu na kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya uamuzi wa mihemko pale wanapofanya makosa ya kiutendaji.

Alisema kuna baadhi ya viongozi na wanasiasa kwa kutumia nyadhifa na vyeo vyao huwanyanyasa walimu bila kujali utu wao ama kufuata sheria, kanuni na miongozo ya kazi hiyo.

Jafo alitoa kauli hiyo juzi, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, alipokuwa akizungumza na walimu kwenye maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani pamoja na miaka 25 ya kuanzishwa kwa chama chao (CWT) hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jafo alisema kila kiongozi anatakiwa kufuata sheria za nchi zilizowekwa kwa kuheshimu haki na wajibu wa mwalimu kwa kujali utu na kazi zao, huku akiwahimiza walimu kuipenda kazi hiyo, licha ya vikwazo wanavyokutana navyo na kuwataka kutimiza wajibu wao kwa kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema kada hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo upungufu wa nyumba za walimu mijini na vijijini.

Alisema hali mbaya vijijini husababisha walimu wengi kutovutiwa kwenda kufanya kazi katika maeneo hayo.

Seifa alisema changamoto nyingine ni madeni ya likizo, matibabu na kupanda kwa madaraja.

Naye Rais wa chama hicho, Leah Ulaya, alisema CWT inaidai Serikali Sh bilioni 66, ambazo ni deni la walimu, ambapo alimuomba Waziri Jaffo kufikisha kilio cha walimu kwa Serikali na kulishughulikia kwa wakati deni hilo, ili walimu wapate stahiki zao.

Katika maadhimisho hayo, CWT ilikabidhi Sh milioni 10 kwa ajili ya rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kisiwani Ukara Septemba 20, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles