27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wamiliki casino waanza ‘kuisoma namba’

Na AGATHA CHARLES –Dar es Salaam


HALI ya biashara ya casino inadaiwa kuwa mbaya baada ya kupungua kwa wateja ikiwa ni takribani miezi minne tangu kuanza utekelezaji wa sheria ya ukusanyaji wa kodi katika michezo hiyo iliyoanza mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Inaelezwa kuwa kutokana na sheria hiyo kuanza kutumika tangu Julai Mosi, mwaka huu, wateja wamepungua na kusababisha hata kupunguzwa kwa wafanyakazi wa casino.

Mmoja wa wafanyakazi wa casino moja jijini hapa (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) alisema idadi ya wafanyakazi waliopunguzwa ni wengi na walikuwa wanajiandaa kwenda kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Alisema walianza kupunguzwa miezi michache iliyopita, lakini wengi waliondolewa kazini Oktoba, mwaka huu.

“Wafanyakazi waliopunguzwa ni wengi, unakuta casino nyingine imepunguza karibu watu 100 kulingana na ukubwa wake.

“Tunaungana kwenda kwa Makonda kumweleza hili ili kujua kama kuna ufumbuzi wowote. Shida ni makato anayokatwa mteja baada ya kushinda, hivyo wakikatwa wengine hawarudi,” kilisema chanzo hicho.

MTANZANIA Jumapili lilifika Casino ya Le Grande iliyopo Dar es Salaam, lakini halikufanikiwa kuonana na uongozi kwa madai mhusika aliyetajwa kwa jina moja la Mariam hakuwapo.

Mwandishi wa habari hii alitakiwa kuacha mawasiliano kwa madai wakiwa tayari watamtafuta jambo ambalo halijatokea hadi sasa.

Hata hivyo, alizungumza na mmoja wa wafanyakazi wa casino hiyo (jina lake linahifadhiwa) kuhusu suala hilo, lakini alisema liko katika majadiliano kwa sababu anaona kuna mazungumzo ingawa hakutaka kusema ni kati ya upande upi na upi.

“Naona suala hilo linajadiliwa, kuna mazungumzo hivyo uongozi ndio unaweza kuzungumzia hilo,” alisema.

MTANZANIA Jumapili pia liliutafuta uongozi wa Casino ya Las Vegas inayodaiwa kukumbwa na dhahama hiyo ya upungufu wa wateja, lakini nako mwandishi alitakiwa kuacha mawasiliano kwa madai kuwa atatafutwa.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa Las Vegas alimweleza mwandishi kuwa suala hilo wanapaswa kuulizwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kwa sababu wao ndio wana nafasi ya kuzungumzia yote.

“Sisi tunafanya kazi hatujafunga, lakini wanaopaswa kulizungumzia hilo ni Bodi ya Michezo ya Kubahatisha,” alisema.

MTANZANIA Jumapili lilifika ofisi za bodi hiyo kwa siku tatu katika wiki mbili pasipo kukutana na Kaimu Mkurugenzi, James Mbalwe.

Katibu Muhtasi wa Mbalwe alisema alipewa maagizo kuwa suala hilo liko ngazi ya juu na wanaopaswa kulizungumzia ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au wizara inayohusika na mchezo huo.

“Mkurugenzi kanituma nikwambie suala hilo linapaswa kuzungumzwa na TRA au wizara maana ndiyo liko ngazi hiyo,” alisema.

Kabla ya taarifa hiyo, katibu muhtasi huyo alilieleza gazeti hili kupitia mmoja wa wafanyakazi wa ofisi hiyo kuwa suala hilo lipo na linajulikana, hivyo liko katika ngazi ya mazungumzo likihusisha TRA na wadau wengine.

“Hilo suala la kupungua wateja na changamoto nyingine linajulikana, lakini kwa sasa liko ngazi ya mazungumzo na TRA wanahusika. Hivyo tusubiri zikishuka taarifa ngazi ya kwetu zitatolewa tu,” alisema mfanyakazi huyo.

Pia gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, ambaye alisema kodi hizo ni kwa mujibu wa sheria iliyoanza kutekelezwa Julai Mosi, mwaka huu.

“Ni sheria mpya iliyopitishwa bungeni, anayecheza casino anakatwa asilimia anaposhinda na akishindwa mchezeshaji analipa asilimia hizo TRA. Viwango vyao vya ulipaji viko tofauti. Hiyo ni kama kukata kodi kipato kama ambavyo wafanyakazi nao wanalipa kodi,” alisema Kayombo.

Pia alisema wanaocheza michezo ya casino wanaposhinda wanakatwa asilimia 12 ya walichokipata huku wale wa michezo mingine ya kubahatisha wanakatwa asilimia 20 tofauti na awali ilivyokuwa asilimia 18.

Kuhusu wamiliki wa michezo hiyo, alisema wale wa casino wanakatwa asilimia 18 huku wale wa mitandaoni wakitakiwa kulipa asilimia 25 ya wanachokizalisha.

Alipoulizwa iwapo kuna majadiliano yoyote kuhusu suala hilo, alisema hiyo ni sheria hivyo kodi ni lazima ikatwe.

“Kimsingi kodi inatakiwa, pato lazima likatwe kodi. Wigo wa kodi ni mdogo, kipengele hicho kilikuwa hakijaanza kutozwa, Julai Mosi imeanza kutumika,” alisema Kayombo.

 

ALICHOTABIRI ABBASS TARIMBA

Itakumbukwa kuwa wakati wa mapendekezo ya bajeti, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu, Abbass Tarimba, aliwahi kuzungumza na gazeti hili kwa kutoa angalizo la ongezeko la kodi katika michezo ya bahati nasibu.

Alisema uamuzi wa kuongeza kodi unaiangusha sekta hiyo na inaweza kuzuia uwekezaji mpya katika michezo hiyo.

Tarimba alisema sekta hiyo imeajiri watu 15,000 lakini kutokana na ongezeko la kodi, kuna hatari ya kupunguzwa kwa wafanyakazi wengi ili wawekezaji wamudu uendeshaji.

Alisema kila sekta ina wataalamu wake na kitendo cha Serikali kuongeza kodi katika sekta hiyo alikitafsri kuwa huenda haipendi kuendelea na michezo ya kubahatisha.

“Sababu zinazotolewa kwamba kodi inapandishwa ili kuongeza mapato ya Serikali bila ya kuangalia chanzo chenyewe cha kodi kinaboreshwaje, maana yake ni kwamba inataka kumkamua ng’ombe bila ya kumpa majani.

“Ukiangalia kwenye michezo ya bahati nasibu, watu nafikiri hawajui njia za uendeshaji wake, mtu kama hajui njia hizo atakuja na namba tu, lakini hawezi akajua kwamba athari ya kutoza kodi kama ambavyo inapendekezwa maana yake ni kwamba waendesha michezo ya bahati nasibu aidha waache au wadanganye,” alisema.

Pia alisema fedha yote inayokusanywa katika michezo ya bahati nasibu kwa utaratibu wa sasa ni kwamba Serikali inachukua asilimia sita moja kwa moja kabla ya matokeo na ulipaji wa zawadi haujafanyika.

“Kwa mfano katika kila shilingi 100, kuna shilingi sita inachukuliwa na Serikali, hii ni tofauti na michezo mingine ya kubahatisha. Kwa mfano kuna kitu kinaitwa ‘taxable revenue’, hii katika sekta ni zile fedha unazozipokea ukiondoa malipo ya zawadi, hivyo kinachobakia ndicho kinaitwa ‘taxable revenue’ na mfumo huu upo duniani kote, lakini  kilichopo hapa nchini wanachukua fedha ghafi.

“Swali linakuja sasa hivi wameongeza na kufika asilimia 10, maana yake kwa kila shilingi 100, shilingi 10 inachukuliwa na Serikali kabla ya matokeo bado, sasa kama matokeo yametokea na watu wamekula zaidi ya asilimia 90, nini kitatokea? Je, mwekezaji atafute wapi fedha ili aweze kuwalipa hao wachezaji?” alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles