26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 8, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JAFO AONYA BARABARA ZENYE MASHIMO TEMEKE

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amewatahadharisha watendaji wa Manispaa ya Temeke kuhakikisha wanasimamia miradi ya ujenzi wa barabara na kusisitiza kwamba, hatarajii kuona barabara zenye mashimo.

Jafo alitoa kauli hiyo alipokuwa akikabidhi jengo lenye maabara ya kupima kiwango na ubora wa vifaa vya ujenzi katika Manispaa ya Temeke, lililojengwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Alisema maabara hiyo, ambayo ina uwezo wa kutumiwa na watumishi 50 kwa wakati mmoja na jengo la maabara ya kupima kiwango cha lami na vifaa vingine vya ujenzi, imejengwa kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa barabara za manispaa hiyo unakuwa wa kiwango cha juu.

“Kuwapo kwa maabara hii ya kisasa ni suluhisho kwa watendaji ambao wanafanya shughuli za ujenzi. Sitarajii baada ya muda kuona barabara zilizojengwa zina mashimo mashimo, nategemea katika siku zijazo tutapata barabara zenye viwango,” alisema Jafo.

Mbali na hilo, Waziri huyo alisema mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuboresha mipango miji na majengo makubwa katika kipindi hiki mpaka 2020 yanaweza kusababisha wageni wanaoingia katika jiji hilo kupotea.

Jafo alisema kupitia Benki ya Dunia, wanatekeleza mradi wa kuboresha jiji hilo kwa kujenga barabara za viwango vya lami na zenye taa, ujenzi wa mitaro ya kisasa na mpangilio wa mji.

“Natamani kuwapoteza watu watakaofika Dar es Salaam 2020, wakifika hapa wakute mabadiliko makubwa, mpangilio wa mji wa kisasa na kazi hii imeshaanza,” alisema.

Awali Mratibu wa Mradi huo katika Manispaa hiyo, Edward Haule, alisema katika Manispaa hiyo wametengewa Sh. bilioni 260 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu na kwamba Sh bilioni 1.4 zimetumika katika jengo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles