MURUGWA THOMAS
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jaffo amewaonya wakuu wa idara wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji nchini ambao hawatimizi wajibu wao kazini kuachia ngazi mapema nafasi zao zichukuliwa wenye uwezo wa kufanya kazi.
Onyo hilo lilitolewa na Jaffo juzi mjini Tabora alipokutana na watumishi wa Manispaa ya Tabora katika ziara yake mkoani hapa.
Alisema baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri wamekuwa hawajiwezi na wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea wanapaswa kuachia ngazi kupisha walio chini yao.
Alisema watumishi wote wakiwamo wakuu wa idara wanatakiwa kufanya kazi kwa malengo kwa sababu serikali ya awamu ya tano inataka tija katika utendaji kazi na si vinginevyo.
Waziri Jaffo alisema watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na umakini waweze kuacha alama isiyosahaulika katika utumishi wao kwenye maeneo yao ya kazi walipo ajiriwa.
Waziri alisema baadhi ya watumishi wa Manispaa ya Tabora si waaminifu kwa vile wamekuwa wakitumika kuhujumu mapato na kusababisha makusanyo kuwa kidogo kila mwezi wakati kuna vyanzo vingi.
Katika kuhakikisha hilo linatatuliwa alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kuunda tume ya kufuatilia vyanzo hivyo hasa vibanda na vitegauchumi vingine vilivyopo kusaidia kuongeza mapato.
Jaffo katika ziara hiyo alikagua ujenzi wa jengo la Hospitali ya Wilaya ya Tabora, ujenzi wa Kituo cha Afya Ipuli na ujenzi wa barabara zinazojengwa kwa lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia zenye urefu wa kilomita 15.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema amepokea maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Jaffo na kwamba kwa kushirikiana na kikosi kazi chake watayafanyia kazi.
Mwanri alisema jukwaa la fursa za biashara na uwekezaji lilifanyika mkoani humo limekuwa la manufaa makubwa kwani hivi sasa baadhi ya wawekezaji wameanza kujitokeza kuweka katika kilimo.
Alisema kila wilaya imejipanga katika suala zima la uwekezaji katika viwanda.
RC alisema wakati Sikonge imewekeza katika kuchakata asali, Urambo kutajengwa kiwanda cha tumbaku, Nzega machinjio ya kisasa na kiwanda cha nyama huku Igunga itawekeza katika kukoboa npunga na uchambuaji pamba.