TEHRAN, IRAN
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Iran amemshambulia Rais DonaldTrump baada ya kutangaza hatouchukulia hatua uongozi wa Saudi Arabia kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi yaliyofanyika katika ubalozi mdogo wa ufalme huo mjini Istanbul, Uturuki mwezi uliopita.
Katika ujumbe wa Twitter uliochapishwa juzi usiku Mohamed Javad Zarif alisema tangazo la Trump lililoishutumu Iran kwa maovu chungu nzima ni la aibu dhidi ya mauaji yanayofanywa na Saudi Arabia.
Zarif pia alifanya masihara kwa kusema pengine hata Iran imehusika na moto wa California kwasababu hawakusaidia kuifyeka misitu kama wanavyofanya Finland.
Waziri huyo alikuwa akielekeza ujumbe wake huo katika matamshi ya hivi karibuni, ambayo Rais Trump alisema kufyeka misitu kunazuia moto nchini Finland na hatua kama hiyo ingesaidia katika jimbo la California endapo ingechukuliwa.