ZURICH, USWISI
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA),Gianni Infantino, amependekeza kuongezwa kwa timu za mataifa 16 kutoka 32 zinazoshiriki michuano ya Kombe la Dunia.
Idadi hiyo itafanya kuwapo kwa timu 48 ambazo ni zaidi ya ahadi yake ya awali alioitoa katika kampeni za urais wa Fifa ambapo alitaka michuano hiyo kushirikisha jumla ya timu 40.
Kwa mujibu wa Infantino (46), anaeleza kuwa mataifa 16 yataondolewa katika mzunguko wa kwanza na kubakia mataifa 32 yatakayoshiriki hatua ya makundi ikifuatiwa na hatua zaidi ya mtoano.
Infantino alisema uamuzi wa kupanua michuano hiyo mikubwa duniani inatarajia kufanyika Januari mwakani.
“Tupo mbioni kutafuta njia sahihi ya kuboresha michuano hii na kabla ya kufika katika uamuzi, kwanza tutafanya mdahalo mwezi huu wa kujadili hoja hii.
Infantino alisema kwa sasa timu 32 kutoka katika mataifa mbalimbali zitashiriki katika hatua za awali za mtoano na washindi kujiunga na timu 16 washindi wa hatua ya makundi.
“Kwa sasa tunaendelea na utaratibu wa kawaida wa Kombe la Dunia kwa kuwa na timu za mataifa 32, lakini hapo baadaye tunatarajia kuwa na timu 48.
“Wazo la Fifa ni kuendeleza soka katika mataifa yote, dunia ni kubwa hivyo tunataka kufanya mashindano haya yawe zaidi na yalivyokuwa hapo awali,” alisema Infantino ambaye alichukua nafasi ya Rais wa Fifa wa zamani, Sepp Blatter, Januari 26, mwaka huu.
Infantino aliongeza kuwa wazo hilo litapanua mashindano hayo kwa kuwa yatashirikisha mataifa ambayo hayakupata nafasi hapo awali.
Katika wazo hilo jipya, inadaiwa huenda ikatokea England kucheza dhidi ya Iceland katika mzunguko wa kwanza kama England hawakufuzu moja kwa moja.