NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
UPATIKANAJI wa Elimu bora hapa nchini umekuwa ni changamoto kubwa kwa sababu ya ubovu wa miundombinu , uhaba wa vyumba vya madarasa, maabara na vifaa muhimu kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kusoma kwa umakini.
Zipo baadhi ya shule hasa zilizopo pembezoni mwa miji ambazo zilijaribu kutumia mbinu mbadala kwa kutandika mikeka au kuweka mawe ili wanafunzi wake waweze kukaa chini na kuendelea na masomo kama kawaida.
Hali hiyo ilikuwa ikisababisha elimu kuzidi kudidimia kwa sababu ya wanafunzi kukosa usikivu na walimu kushindwa kuwadhibiti wanafunzi hao ambao wengine walikuwa wakikaa chini ya miti.
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli, ilipoingia madarakani iliona kwa karibu kadhia hiyo na kuamua kuipa elimu kipaumbele ili kuweza kutokomeza changamoto mbalimbali zilizokuwa zinainyemelea sekta hiyo muhimu.
Rais Magufuli kwa kuanzia alitangaza elimu bure ili kila mwanafunzi apate fursa ya kusoma kwa kuwasaidia wazazi kuhakikisha watoto wao wanaendelea na elimu kuanzia msingi hadi sekondari.
Pia serikali ilianzisha kampeni maalumu ya kukusanya madawati kuanzia ngazi za kata, wilaya hadi mkoa ili kila shule iweze kuondoa changamoto ya wanafunzi wao kukaa chini.
Wadau mbalimbali wa elimu zikiwemo asasi na watu binafsi walijitokeza kuunga mkono agizo hilo la serikali kwa kujitolea madawati ili kuondoa upungufu uliopo ambao ulikuwa unasababisha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
Benki ya NMB nao ni miongoni mwa wadau ambao waliahidi kutenga asilimia 1 ya mapato yao ili waweze kununua madawati.
Benki hiyo iliahidi kutoa Sh bilioni 1.5 katika kipindi cha miaka mitano ambazo zitatumika kununua madawati kwa shule 71 za msingi na sekondari.
Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, anasema benki hiyo iliona haja ya kuhakikisha inatoa msaada wa elimu kama kipaumbele kwa sababu elimu ndiyo msingi wa kila kitu.
Anasema msaada huo ni sehemu ya ahadi ambayo waliilitoa mwaka 2014 ya kusaidia jamii kupitia sekta ya elimu na kupitia sera ya kampuni hiyo ya Corporate Social Responsibility ni kutenga sehemu ya faida wanayoipata kila mwaka kwa ajili ya kutoa misaada.
“Tuliahidi mwaka 2014 kuwa NMB tutashirikiana na serikali katika jitihada za kukusanya madawati ambapo tulitoa ahadi ya madawati 15,000 na mpaka sasa tumekwishakabidhi madawati 10,000,”anasema Ineke.
Anasema ana imani mkakati wa serikali wa kukusanya madawati utasaidia kuondoa adha walizokuwa wakikumbana nazo wanafunzi kwenye shule mbalimbali hapa nchini.
Pia anasema wamefanikiwa kuiwezesha Serikali kompyuta 250 ambazo zitasambazwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari nchini ili kuweza kuwapa fursa wanafunzi kujifunza somo la teknolojia ambalo hivi sasa linashika kasi katika soko la dunia.
“Ni mkakati wetu wa kuendeleza sekta mbalimbali nchini, kuwawezesha hawa vijana ni sawa na kuiendeleza dunia hivyo kizazi cha sasa kinatakiwa kijengewe mazingira ya kuuzika kwenye Soko la Biashara la Afrika Mashariki,”anasema Ineke.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, anasema NMB ni moja ya wadau ambao wameiwezesha serikali kupiga hatua katika ukusanyaji wa madawati nchini na kutokomeza adha ya wanafunzi kukaa chini.
Anasema jitihada za serikali ni kuona kila shule kuanzia ngazi ya kata hadi taifa inakuwa na madawati ya ziada ili wanafunzi waweze kupata elimu bora na si bora elimu.