31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO: WANASIASA, VIONGOZI WA DINI, HAWANA KINGA KUTOKAMATWA

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA 

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amewaambia askari wa jeshi lake kuwa wanasiasa, viongozi wa dini na watu maarufu hawana kinga ya kutokamatwa ikiwa wamefanya uhalifu.

Pia amekemea vikali tabia ya ubambikiaji kesi na ukiukwaji wa maadili ya jeshi hilo ambazo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya askari.

IGP Sirro aliyasema hayo juzi jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao na askari wa Jeshi la Polisi.

Katika maelezo yake, alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya watu wanaodai kubambikiwa kesi na polisi, huku wengine wakidaiwa kutoa siri za raia wema wanaotoa taarifa kwa jeshi hilo.

“Nilikuja kufanya ukaguzi, mambo makubwa niliyowakumbusha ni wajibu wao. Moja ya wajibu wao mkubwa ni kuelewa wao ni watumishi wa umma, hivyo wanapaswa kufuata masharti ya umma.

“Kutenda haki ni suala la msingi sana kwetu bila kuangalia uwezo wa mtu, cheo, rangi, kumekuwa na malalamiko sana,  watu wanasema tunabambika kesi, wengine wanasema tunatoa siri za raia wanaotupa taarifa, askari yeyote atakayekiuka maadili akibainika, hatua kali za kisheria dhidi yake zitachukuliwa.

“Kimsingi nasisitiza suala la nidhamu ndani ya jeshi, kama mnavyofahamu jeshi bila nidhamu kazi zetu haziwezi kwenda,” alisema IGP Sirro.

Akizungumzia kuhusu kamatakamata ya baadhi ya viongozi wa siasa, IGP Sirro alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria, hivyo wanapopata taarifa za mtu kufanya uhalifu lazima wamkamate.

“Kwani mwanasiasa hawezi kuwa mhalifu, nilishasema sana siasa siyo kinga, tunapewa taarifa na tukiona ukweli wa ile taarifa, kama mtu ni mtuhumiwa siwezi kumwacha kwa sababu ni mwanasiasa, kiongozi wa dini au mtu maarufu, tutamkamata tutamhoji, tutampekua na tukiona hahusiki tunaachana naye.

“Tukikuta anahusika tunampeleka mahakamani kwani hakuna aliye juu ya sheria,” alisema IGP Sirro.

Aidha IGP Sirro alitumia nafasi hiyo kulipongeza jeshi hilo mkoani hapa na kusema kuwa takwimu za makosa makubwa zimepungua, ikiwa ni pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Alisema kuwa amesisitiza kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi za vijiji kuhakikisha wanakuwa makini na kushirikiana na wananchi kuzuia matukio mbalimbali akitolea mfano mauaji yaliyokuwa yakitokea Kibiti mkoani Pwani.

“Wengi wanauliza habari ya Kibiti, Kibiti iko shwari na itaendelea kuwa shwari, tunaendelea kuwakamata kwani wengine wamekimbilia mikoa mbalimbali na nilishasema kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu ni lazima ujue tutakushughulikia kwa mujibu wa kanuni zilizopo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles