25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO: NCHI INA VIASHIRIA VYA MPASUKO

UDITH NYANGE NA CLARA MATIMO -MWANZA

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema taifa linakabiliwa na viashiria vya mpasuko na mmomonyoko wa msingi wa amani uliojengwa na viongozi waliotangulia.

Alifafanua hoja hiyo kwa kusema hali hiyo inachochewa na kauli au matamko ya vitisho dhidi ya watu wanaotumia uhuru wao wa kutoa mawazo mbadala.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, alisema hayo jana wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama chake.

Kiongozi huyo alisema ufinyu wa demokrasia ni moja ya changamoto inayolikabili taifa kwa sasa.

Alisema hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kuamini kuwa maendeleo yanakuja kwa kuminya uhuru wa watu, hususani viongozi wa vyama vya upinzani.

Katika hoja hiyo, Zitto aliwataka wananchi kupaza sauti zao kwa kukemea udikteta kwa lengo la kuilinda amani iliyopo nchini.

“Kauli na matamko ya vitisho na vitendo vya bughudha vimeshamiri kwa wale wanaotofautiana mtazamo na watawala.

“Hii inaashiria mpasuko na mmomonyoko wa msingi wa amani uliojengwa na viongozi waliotangulia na kusababisha athari za uchumi pamoja na kukosekana kwa sauti mbadala ya kuleta marekebisho ya kisera,” alisema Zitto.

 

MDORORO WA UCHUMI

Katika hatua nyingine, Zitto alielezea mdororo wa uchumi kwa kusema tayari nchi imeanza kuona madhara hasi ya kuminywa kwa demokrasia.

Alisema mtazamo huo unatokana na vitendo vya kamatakamata ya viongozi wa vyama vya upinzani, ambao ni wawakilishi wa wananchi.

Zitto alisema vitendo hivyo vimechangia kuporomoka kwa mshikamano uliokuwa umeanza kujengeka ndani ya nchi bila kujali itikadi za vyama.

Alisema kuporomoka kwa mshikamano kumejenga chuki na matokeo yake hali hiyo imesababisha mdororo wa kiuchumi.

“Mwaka 2016 kilimo cha mazao kilikua kwa asilimia 1.4 tu kutoka asilimia 2.2 mwaka 2015 na asilimia 4 ya miaka iliyopita.

“Ukichukua kasi ya ongezeko la idadi ya watu Tanzania ya asilimia 2.8 kwa mwaka, maana yake ni kwamba mwaka 2016 Watanzania tuliongezeka maradufu na  wengi walidumbukia kwenye umasikini kuliko 2015.

“Wakati Serikali inaimba viwanda, mauzo ya bidhaa kwenda nje ya nchi yetu yameshuka sana, Mei 2016 Tanzania iliuza nje bidhaa za viwanda zenye thamani ya dola bilioni 1.5, mwaka ulioishia Mei 2017 Tanzania imeuza nje bidhaa zenye  thamani ya dola bilioni 0.8 tu, anguko la mauzo ni takribani dola milioni 700, sawa na thamani ya ndege 23 za Bombadier Q 400,” alisema.

Pia alisema uagizaji wa bidhaa za chakula kutoka nje umeongezeka kwa asilimia 14 ndani ya mwaka mmoja wa Mei 2016 hadi Mei 2017, kwamba Tanzania imetumia dola milioni 480 kuagiza sukari, nafaka na mafuta ya mawese kutoka nje ya nchi.

Zitto ambaye alisema mauzo ya nje ya zao la pamba yameshuka kutoka dola milioni 52 kwa mwaka 2016 hadi dola milioni 42 Mei, mwaka huu na uagizaji wa malighafi umeporomoka kwa asilimia 25 ndani ya mwaka mmoja kati ya Mei 2016 na Mei mwaka huu.

Alisema takwimu hizi chache zinaonyesha  hali ya nchi si imara na kuna hatari  Watanzania wengi wakatumbukia kwenye umasikini zaidi, hivyo alishauri ni vyema viongozi wakaacha vitisho kwa wote wanaotumia uhuru wao wa kutoa mawazo mbadala nchini, kuimarisha uhuru wa kidemokrasia bila kujali tofauti za kisiasa, kiuchumi, kidini na kikabila ili kulinda demokrasia na kusukuma mbele maendeleo.

“Wananchi wenzangu, ni muhimu  kuendelea kupaza sauti kupinga kubanwa kwa demokrasia, hatupaswi kabisa kukaa kimya, huu ni wajibu wetu wa kizalendo, tusiwaachie nchi wahisani, tusiache kupaza sauti juu ya udikteta ili kulinda amani yetu.

“Vyama vya upinzani vinaongoza halmashauri zaidi ya 35 nchini, kuzuia mikutano ya hadhara ni uvunjifu wa katiba, lakini pia ni kuondoa uwajibishaji, tunaongoza halmashauri hizo kutoka kwa CCM ambao ni wapinzani wetu katika maeneo hayo,” alisema Kabwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles