KUTOKANA na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kupoteza maisha ya watu katika maeneo ya Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, pamekuwapo mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi, kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi katika kukabiliana na hali hii.
Wakati mitazamo tofauti ikiibuka kuhusu kukabiliana na uhalifu, wananchi walio wengi wakiwamo wanasiasa wamekuwa hawatoi ushauri na mwelekeo utakaowasaidia polisi wetu kuibuka kidedea.
Pamoja na Jeshi la Polisi kushauriwa kushirikiana na raia, lakini limekuwa likilaumiwa sana kuliko uhalisia kwamba limeshindwa kabisa, huku baadhi ya wananchi wakiendelea kuwa na mawazo mgando kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndicho chombo pekee kinachoweza kutoa suluhisho na kusahau kwamba hata JWTZ ni binadamu wanaotumia damu.
Katika makala yangu yaliyopita nilitoa ushauri kwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP) Sirro kuunda kikosi imara cha upelelezi chenye uadilifu na uwezo mkubwa katika kubaini vitendo vya uhalifu kabla havijaleta madhara katika jamii.
Hata hivyo kuna haja Jeshi la Polisi kutumia teknolojia mpya kulingana na mabadiliko ya dunia yanayosababisha uhalifu kutekelezwa kimkakati
Polisi wetu wanaweza kujifunza kutoka Idara ya Polisi katika Jiji la Chicago nchini Marekani ambalo limeamua kutumia mikakati ya teknolojia kubwa na zana za kisasa kutokana na kuongezeka vitendo vya mauaji na magenge yanayofanya ghasia.
Afisa Mnadhimu wa Polisi jijini Chicago, Eddie Johnson wakati akizungumza na waandishi wa habari Februari Mosi mwaka huu, alisema kuwa, Idara ya Polisi kwa sasa inatumia mikakati ya teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na uhalifu.
“Tumebadilisha utamaduni wa kupambana na uhalifu katika idara ya Polisi ya Chicago,” Johnson alisema, huku akiongeza kuwa anaamini teknolojia itasababisha kukamata wahalifu wa ghasia na hivyo kupunguza idadi ya mauaji na mashambulizi.
Afisa huyo alionesha namna maafisa wa polisi watakavyotumia haraka iwezekanavyo programu za kompyuta ili kusoma na kutambua ni wapi pamefyatuliwa risasi huku wananchi wakionyeshwa namna mfumo wa kompyuta utakavyoweza kutambua mara moja ni wapi kuna ghasia.
Kiongozi huyo aliendelea kueleza namna idara ya polisi imepanua teknolojia ijulikanayo ‘‘ShoSpotter’’ ambayo inatumika katika miji mikubwa ili kusaidia kutambua uhalifu ambapo zaidi ya vitambuzi (sensors) 100 vimewekwa huku vikiwa vimeunganishwa kwenye simu za viganjani (smartphones) ambazo huunganishwa kwenye kompyuta na kutambua ndani ya sekunde chache mwelekeo wa bunduki ilikotumika.
Wakati huohuo polisi wameongeza idadi ya kamera zinazoongozwa kwa ‘remote’ pamoja na teknolojia ya kutambua bunduki katika miji hiyo huku vifaa hivyo vikiwa vimewekwa kwenye mfumo ujulikanao ‘Strategic Decision Suport Center’ ambapo kila kituo cha polisi kimeunganishwa.
Pia kila kituo kina mfumo wa kompyuta ujulikanao Hunch Lab ambao hujazwa taarifa za ukamataji na data nyingine zinazoweza kubashiri maeneo ambayo uhalifu unaweza kujitokeza.
Jiji la Chicago limekuwa kitovu cha ghasia zinazohusisha matumizi mabaya ya bunduki ambapo inakadiriwa mwaka jana pekee takribani watu wapatao 762 waliuawa ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya miji miwili ya New York na Los Angeles.
Mafanikio ya polisi jijini Chicago katika matumizi ya teknolojia ni matokeo ya Serikali ya Marekani kuwekeza vyakutosha katika chombo hicho, ambapo hata Serikali ya Tanzania haina budi kufanya hivyo haraka ili kukabiliana na uhalifu.
Hata hivyo hakuna mazingira yoyote yawe ya kisiasa kama inavyohisiwa huko Kibiti na Rufiji, au mazingira ya kiuchumi na kijamii yanayoweza kupindua zana ya uhalifu kuwa halali.