Na Ramadhan Libenanga – Morogoro
MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amesema mambo yanayotokea katika matukio ya mauaji ya mfululizo wilayani Rufiji, Ikwiriri na Kibiti mkoani Pwani, hawawezi kuyazungumzia hadharani kutokana na sababu za kiusalama.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitokea bungeni mjini Dodoma kusikiliza hotuba ya makadirio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
IGP Sirro alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuyataja mambo hayo kupitia vyombo vya habari kutokana na mambo ya kiusalama na mikakati waliyojiwekea.
“Sio kila jambo la usalama linapaswa kutangazwa, hasa wakati huu wa operesheni ya kuwasaka wauaji hao.
“Kilichopo sasa ni kwamba polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama tunaendelea kuhakikisha hali ya amani inarudi maeneo ya Kibiti,” alisema.
Sirro alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya watu watatu kuuawa Kibiti kwa kupigwa risasi saa nane ya usiku wa kuamkia juzi.
Watu hao waliuawa katika Kijiji cha Nyamisati, ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya mauaji mkoani humo yaliyotokea kwa kufuatana ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya watu wengine wanne kuuawa, mmoja kutekwa na mwingine kujeruhiwa kwa risasi na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakazi wa Kibiti, wauaji hao waliwaua wanakijiji watatu; Hamid Kidevu, Yahya Makame na Moshi Machela na kutokomea na maiti zao kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, aliliambia MTANZANIA Jumapili kwa simu jana kuwa licha ya juzi kutuma kikosi cha askari katika eneo la tukio kuwasaka wauaji hao na maiti hizo, lakini hadi sasa bado hazijapatikana.
Lyanga alisema bado hajapata taarifa yoyote ya ziada kuhusu tukio hilo.
“Sina taarifa mpya, taarifa ni zile zile kama nilizozitoa jana,” alisema Lyanga.
Mbali na taarifa hiyo ya Lyanga, naye Sirro alizungumzia mtindo mpya wa mauaji hayo yaliyotokea juzi baada ya maiti za wanakijiji hao kutopatikana kwa kusema kuwa polisi nao wanahakikisha wanafuatilia kwa ukaribu jinsi wauaji hao wanavyobadilisha mtindo wao wa kutekeleza uhalifu huo.
Pia alivitaka vyombo vya habari hapa nchini kuacha kuandika habari za uchochezi na kuwatia hofu wananchi wanaoishi maeneo ya Rufiji na Kibiti.
Alilalamika kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari vinaandika habari za mauaji hayo kwa lengo la kusherehesha vyombo vyao.
“Ndugu zangu wanahabari, Jeshi la Polisi linatambua kwa kiasi kikubwa mchango wenu katika kuelimisha jamii, hasa masuala mbalimbali yanayohusu nchi yetu, lakini imekuwa tofauti na habari za mauaji ya Kibiti zinavyoripotiwa katika vyombo vyetu si kizalendo,” alisema.
Siro alisema kuwa vyombo hivyo (sio MTANZANIA Jumapili) vimekuwa vikiripoti kuonyesha kama maeneo ya Rufiji, Kibiti na Ikwiriri ni uwanja wa vita na hali hiyo inawatia hofu waishio uko na wale wanaotamani kwenda kuishi.
Alisema wamekuwa wakishuhudia vyombo vya habari vikiripoti habari za Kibiti kwa kuonyesha watu waliojeruhiwa vibaya wakiambatanisha na silaha za kivita kitu ambacho ni kinyume na uhalisia.
Aliwakumbusha wanahabari kuwa wanapoandika masuala ya kiusalama, wanapaswa kuzingatia ukweli wa taarifa kutoka kwa vyombo husika, ikiwa pamoja na kutanguliza uzalendo ili kuepusha athari zinazoweza kutokea kutokana na taarifa zisizo na uchunguzi wa kina.
“Epukeni kuandika habari zenye sura ya ushabiki katika mauji ya Kibiti na maeneo mengine ili kuelimisha jamii,” alisema.
Tangu mauaji hayo yatokee inadaiwa kuwa watu takriban 38 wameshapoteza maisha.
Baada ya mauaji hayo kuendelea kutokea mfululizo mkoani humo, Rais Dk. John Magufuli, alifanya mabadiliko ya kumwondoa IGP Ernest Mangu katika nafasi hiyo na kumteua Sirro aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwa IGP mpya.
Baada ya kuteuliwa, Sirro aliweka mikakati ya kuwabaini wauaji hao na kuwachukulia hatua.
Siku nne zilizopita, Sirro alifika mkoani Pwani na kuzungumza na wazee ili kujua kiini cha mauaji hayo.