RIPOTI YA PILI YA MAKINIKIA KUTIKISA MJADALA WA BAJETI

0
742
Rais, Dk. John Magufuli

 

 

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

RIPOTI ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa madini (makinikia), ambayo inatarajiwa kuwasilishwa kesho kwa Rais, Dk. John Magufuli, huenda ikatikisa mjadala wa Mapendekezo ya Serikali ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mwaka 2017/18.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kamati inayoundwa na wachumi na wanasheria ambayo pamoja na mambo mengine itamshauri Rais Magufuli hatua za kuchukua katika masuala ya kisheria, ikiwamo mikataba katika sekta ya madini na masuala ya kiuchumi, inawasilishwa wakati ambao wabunge wanatarajia kuanza kuyadili mapendekezo ya bajeti kesho.

Tayari wabunge, hasa wa upinzani, wamejiandaa kuikosoa bajeti hiyo katika maeneo mbalimbali, hasa uamuzi wa Serikali kuhamishia ada ya leseni ya magari (Road License) kwenye mafuta hatua ambayo wanadai itawaongezea mzigo wananchi wa kawaida, huku wengi wao wakiwa hawamiliki magari.

Kwa sababu hiyo, ripoti hiyo inatazamwa kuibua mjadala mpya katika sekta ya madini, hatua ambayo inavuta hisia kwamba huenda ikatikisa mjadala wa bajeti ya 2017/18.

Ingawa baadhi wanaona kwamba ripoti hii haitaweza kuathiri mwenendo wa mjadala wa jambo kubwa kama bajeti ambalo linawagusa watu wengi, lakini itakumbukwa ripoti ya kwanza iliyowasilishwa siku 16 zilizopita na wanasayansi ambao walichunguza kiwango cha madini kilichomo katika mchanga unaosafirishwa nje ya nchi jinsi ilivyoibua mjadala mkubwa si tu kile kilichoelezwa ndani ya ripoti bali uamuzi aliochukua Rais Magufuli.

Si hilo tu, itakumbukwa pia mjadala wa ripoti hiyo ambao ulikoma mwishoni mwa wiki baada tu ya bajeti ya mwaka 2017/18 kuwasilishwa bungeni, ulidumu kwa muda katika vyombo mbalimbali vya habari na kwenye mitandao ya kijamii na hata kuzima baadhi ya hoja.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa,  taarifa ya kamati ya pili ya wachumi na wanasheria iliyofanya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga wa madini yaliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini itakabidhiwa kwa Rais Magufuli kesho.

“Tukio hili litarushwa hewani moja kwa moja (mubashara) kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu kuanzia saa 3:30 asubuhi.

“Wananchi wote mnakaribishwa kufuatilia matangazo hayo kupitia vyombo mbalimbali vya habari ama simu zenu za mikononi kwa kutembelea tovuti rasmi ya Ikulu,” ilifafanua taarifa hiyo.

Wakati Ikulu inatoa taarifa hiyo, ikumbukwe tangu Serikali ilipowasilisha bungeni mapendekezo yake ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18, Alhamisi iliyopita, si tu wabunge hata jamii kwa ujumla imekuwa na maoni mbalimbali yanayokinzana kuihusu.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekwishatamka bayana kwamba itatoa maoni yake leo baada ya kukesha siku mbili wakiichambua bajeti hiyo.

Hata hivyo, kuwasilishwa kwa taarifa ya pili ya uchunguzi wa madini kwa rais kesho, kunatazamwa kuibua mambo mazito, hasa yatakayogusa masuala ya sheria kwa maana ya mapitio ya sheria ya sasa ya madini na mikataba ili iweze kuendana na mazingira ya sasa.

Wakati wa hitimisho la mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Naibu Waziri, Dk. Medard Kalemani, aliwaambia wabunge waliohoji kuhusu sheria ya madini na mikataba kuwa suala hilo waichie kwanza kamati hiyo ya wasomi wa sheria kwamba inaweza ikamshauri rais.

Mbali na hilo la kisheria, udadisi zaidi unadai kuwa taarifa ya pili ya uchunguzi huo inaweza ikaibua mazito zaidi yaliyojikita kwenye mchanganuo wa kiuchumi, hususani kiwango cha fedha ambacho Serikali ama imekipata au kupoteza kupitia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Kutokana na muktadha wa ripoti ya kwanza ambayo ilishuhudia Rais Magufuli akiwaondoa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na viongozi waliokuwa wakiongoza Mamlaka ya Kudhibiti Madini Tanzania (TMAA), macho na masikio ya wengi yamejielekeza kusikia nani atasalimika safari hii na nani hatasalimika.

Ikumbukwe kwamba wakati wa mjadala wa taarifa ya kwanza ya uchunguzi wa makinikia, Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii uliosomeka; “Tulikosea njia tulipopitisha sheria ya madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria, tukajifunga pingu. Nani wa kumlaumu?”

Hoja kama hiyo pia ilizungumzwa na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Tundu Lissu, ambaye amekuwa akihoji matatizo ya mikataba ya madini, miongoni mwake ikiwamo sheria ya madini ya mwaka 1998, ambayo Serikali iliipeleka bungeni kwa hati ya dharura na ikapitishwa ndani ya siku moja.

Ndani ya mitazamo au hisia za kile kinachoitwa hitilafu za kisheria ambazo zimesababisha taifa kuwa na mikataba mibovu ya madini, majina ya wanasheria wakuu wa Serikali (AG) wawili, Andrew Chenge na Jaji Frederick Werema, yamekuwa yakinyooshewa vidole zaidi.

Chenge aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1993 hadi 2005 anatazamwa kuwa na ufahamu au ushuhuda wa mikataba yote mikubwa ya madini ambayo inalalamikiwa kwa sasa ambayo ilisainiwa kati ya mwaka 1994 na 2007.

Wakati Chenge akiwa AG katika kipindi cha utiaji saini mikataba hiyo, chini ya Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa (1995 – 2005), Jaji Werema alikuwa mtaalamu wa sheria katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jaji Werema alishika nafasi hiyo mwaka 1984 hadi 2007 na baadaye kuja kuwa Mwanasheria Mkuu mwaka 2009 hadi 2014, akichukua nafasi ya Johnson Mwanyika aliyestaafu kwa lazima.

Wakati mjadala wa taarifa ya kwanza ya uchunguzi wa makinikia ukiwa bado mkubwa, gazeti la MTANZANIA katika toleo la Aprili 27, lilimkariri Chenge akishangaa kunyooshewa kidole kila mara.

Kwa upande wake, Jaji Werema alisema haoni kama kuna tatizo la kisheria katika mikataba ya madini, isipokuwa kuna watu ambao walikuwa hawafanyi kazi yao sawasawa.

Wakati hayo yakijiri, Kampuni ya Acacia nayo iliipinga taarifa ya kwanza ya kamati ya uchunguzi wa makinikia, ikidai haikuwa sahihi, zaidi ikiomba ufanyike uchunguzi huru ili kupata ukweli.

Katika hatua nyingine, duru za habari kutoka ndani ya Acacia zimeliambia gazeti hili kwamba mmoja wa watendaji wa juu wa kampuni hiyo aliwasili nchini baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya kwanza ya uchunguzi wa makinikia.

Inaelezwa mtendaji huyo ambaye alikuwa akitokea katika mataifa makubwa, alikuja kwa lengo la kutaka kuonana na Rais Magufuli, lakini jitihada zake zilikwama.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni inadaiwa kuwa ujumbe mwingine wa Acacia ulifika nchini na kufanikiwa kukutana na baadhi ya maofisa wa Serikali na haijajulikana mara moja walichokizungumza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here