24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

IGP Sirro ahimiza ushirikiano

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

WANANCHI na Jeshi la Polisi nchini, wametakiwa kupambana na bidhaa bandia kwa kuwa zina madhara katika jamii.

Kauli hiyo iliyolewa mjini hapa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, alipofungua mafunzo kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia kwa maofisa upelelezi wa makosa ya jinai wilaya na mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Akizungumza kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC), IGP Sirro, alisema uhalifu unaohusiana na biashara ya bidhaa bandia, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya, bado ni changamoto zinazovuka mipaka ya nchi.

“Wahalifu kila kukicha, wanabuni mbinu za kuzalisha na kusambaza bidhaa bandia. Biashara hii inaharibu sifa za kampuni halali na inazikosesha Serikali mapato halali na inawadhuru walaji duniani.

“Kwa kushirikiana na mamlaka za kiserikali, operesheni mbalimbali zimefanikisha kukamatwa bidhaa za matumizi ya kawaida, vyakula vya watoto, vifaa vya ujenzi, vipuri na vilainishi vya mitambo na magari.

“Sisi katika Jeshi la Polisi, tumejizatiti kukomesha biashara hii ya bidhaa bandia pamoja na biashara  nyingine zinazoathiri walaji na kuikosesha Serikali na wawekezaji mapato halali,” alisema IGP Sirro.

Pamoja na hayo, IGP Sirro alilitaka jeshi hilo kuanza kubadilika na kufanya kazi kisayansi na kidijitali badala ya kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.

“Elimu hatuwezi kuikwepa katika kupambana na bidhaa bandia, watu wetu wajikite katika masuala ya kitaaluma zaidi kwenye teknolojia kwani vijana wa leo wapo mbali zaidi kitaaluma kuliko tunavyofikiria,” alisema IGP Sirro.

Mkurugenzi wa kudhibiti bidhaa bandia na kumlinda mlaji kutoka Tume ya Ushindani, Godfrey Gabriel, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dk. John Mduma, alisema soko lililojaa bidhaa bandia hufukuza wawekezaji makini.

Alisema Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963, iliyorekebishwa, ndiyo sheria kuu ya kudhibiti biashara ya bidhaa katika soko la Tanzania Bara kwani inaeleza aina mbalimbali za makosa ya kijinai yanayohusisha bidhaa na adhabu zake.

Mwisho.

Ekari 4,000 za uwekezaji zatengwa Kilimanjaro

 

Na UPENDO MOSHA-MOSHI

 

MKOA wa Kilimanjaro, umetenga ekari 4,296 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji, katika wilaya za Moshi na Siha.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi jana, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, aliwataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya mkoa huo, kufika mkoani humo kwa ajili ya uwekezaji.

 

Kuhusu maeneo ya uwekezaji, mkuu wa mkoa alisema Wilaya ya Moshi imetenga maeneo ya Lokolova ambako kuna ekari 140 na ekari 9 ziko eneo la Njia Panda, wilayani humo wakati ekari nyingine 1,676  zimetengwa wilayani Siha.

 

“Pamoja na maeneo hayo, pia zipo ekari nyingine 2,471 zilizo chini ya Chama cha Ushirika cha Lokolova ambazo zinafaa kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali.

 

“Pamoja na kutenga maeneo hayo, bado kunakabiliwa na ukosefu wa miundombinu ya maji, umeme na barabara na yakiwekewa miundombinu hiyo, itakuwa imesaidia kuwavutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Mgwhira.

 

Katika utekelezaji wa agizo la Serikali la uanzishwaji wa viwanda 100 kila mkoa, alisema tayari mkoa huo umefanikiwa kuanzisha viwanda vipya 74 kwa kipindi cha Desemba 2017 hadi Agosti 2018 ambavyo vimezalisha ajira 787.

 

“Kwa upande wa kufufua viwanda, tayari mkoa umewasiliana na taasisi za Serikali na binafsi ambapo viwanda vya Kilimanjaro Machine Tools Manufacturers Ltd, Karanga Footwear, Mamba Myamba Ginger Company vipo mbioni kufufuliwa kupitia Mfuko wa Hifadhi wa PSSSF.

 

”Kati ya viwanda 74 vilivyoanzishwa hadi sasa, viwanda 48 ni vidogo sana, viwanda 23 ni vidogo, viwanda viwili ni vya kati na kiwanda kimoja ni kikubwa, lakini tunaendelea kutekeleza mpango huu wa Serikali,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles