26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

IGP : MWANDISHI ALIYEPIGWA ALIMKABA ASKARI

Na JANETH MUSHI -ARUSHA


MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, amedai mwandishi wa kituo cha redio Wapo, Sillas Mbise, ambaye hivi karibuni video ilisambaa kwenye mitandao ya jamii ikionyesha polisi wakimpiga, alimkaba askari na kujilaza mbele ya kamera.

Kipande cha video kilichosambaa mitandaoni na kuamsha hisia za wadau mbalimbali wa habari nchini, kinaonyesha polisi wakimpiga mateke na ngumi Mbise wakati akitekeleza majukumu yake Agosti 8, mwaka huu, siku ambayo timu ya soka ya Simba ilicheza mechi ya kirafiki na Asante Kotoko ya Ghana.

Akizungumzia tukio hilo akiwa jijini hapa jana, Kamanda Sirro alisema taarifa walizonazo ni kwamba mwandishi alikuwa mbishi, alimkaba askari polisi akitaka kuingia sehemu iliyokataliwa, wakaanza kuvutana.

“Sasa kwa vurugu zile polisi akawa na hasira, mwandishi akawa na hasira na akavua shati lake, suala la msingi tupeleleze, ila nimeagiza kwa sababu ilionekana kuna vurugu amefanya kabla ya kuonekana kwenye ile video.

“Nimeagiza jalada lifunguliwe na wale vijana walioonekana wanampiga nao lazima tupeleleze kwa sababu mambo yote ni ushahidi.

“Kushambulia waandishi wa habari si sahihi, lakini kikubwa Watanzania lazima waelewe, ukimuona mwandishi amevua shati amekaa chini, suala la msingi lazima ujiulize kabla ya hapo kumetokea nini walipoanzia, ni waandishi wote waliokuwa kwenye lile tukio walivuliwa nguo?

“Jambo la msingi wewe hata kama ni mwandishi wa habari, utii wa sheria bila shuruti lazima ufuate, huwa nalisema siku zote waandishi wa habari ukitaka twende vizuri mimi nitii sheria, mwandishi wa habari utii sheria, usipotii sheria, ukakimbia kwenda kujionyesha umeanguka chini umevua shati, haisaidii kwa sababu sheria ziko kuhakikisha tunaishi kwa amani.

“Ukivunja sheria kwa sababu ni mwandishi wa habari ukakimbia kwenye vioo uonekane unafanya nini, hivi polisi ni kichaa, waandishi wangapi walikuwa kule wasipigwe.

“Na nyie waandishi wa habari mna weledi, fanyeni kazi kwa weledi wenu, akikuambia hapa huruhusiwi kupita usipite, usilazimishe.

“Walimpiga kwa sababu alifanya fujo, ndiyo maana nasema suala la utii bila shuruti nikikwambia usifanye hapa, ukifanya kwa nguvu ukazuia, nitakushughulikia na nitakushughulikia kwa mujibu wa sheria.”

 

YALIYOJIRI UCHAGUZI MDOGO

Akizungumzia yaliyojiri wakati wa uchaguzi mdogo wa Agosti 12, alisema ulienda vizuri ingawa kuna matukio madogo madogo yaliyojitokeza.

“Tumeona uchaguzi ulienda vizuri sana, kuna matukio madogo madogo yalijitokeza ya watu kupigana, watu walikuwa na mihemko, majalada yamefunguliwa, upelelezi unafanyika. Ushahidi ukikamilika wenye makosa watapelekwa mahakamani, haijalishi ni chama tawala au vyama vya upinzani, sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

 

UBAKAJI, MAUAJI YA WANAWAKE MTO WA MBU

IGP Sirro, alisema akiwa wilayani Monduli, atatembelea Kata ya Mto wa Mbu ambako kumekuwa kukiripotiwa matukio ya ubakaji na mauaji ya kinyama kwa wanawake.

Alisema baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, kutembelea eneo hilo wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani na kupokea malalamiko hayo, naye anataka kufika katika eneo hilo ili kubaini chanzo.

“Napita naelekea Mto wa Mbu, kama mlivyosikia Waziri wa Mambo ya Ndani alipita pale na wananchi walilalamika kuna matukio ya mauaji, nataka niende kuona tatizo liko wapi, kabla sijaenda kutembelea kituo cha polisi ambacho kina idadi ndogo ya askari,” alisema.

Julai 9, mwaka huu, Ruth Elias, mkazi wa Mto wa Mbu, aliuawa baada ya kubakwa na watu wasiojulikana, matukio yaliyowachosha wanawake wa eneo hilo, ambao walilazimika kufanya shughuli zote za maziko bila kuwashirikisha wanaume kwa madai kuwa ndio chanzo.

Waziri Lugola aligeuka mbogo kuhusu matukio hayo na kusema uongozi wake hautavumilia matukio hayo yaendelee na kumtaka Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi, kuhakikisha taswira nzuri ya mkoa huo haipotei.

Kuanzia mwaka jana hadi sasa, wanawake wanane wanadaiwa kuuawa mkoani hapa.

Kamanda Sirro aliongeza kuwa akiwa wilayani Mbulu, atazungumza na askari pamoja na kutembelea kituo cha polisi wilaya.

“Kikubwa nitakachosisitiza ni nidhamu, kutenda haki na kuhakikisha kwamba wanadhibiti uhalifu,” alisema na kuongeza kuwa suala la kutenda haki ni la msingi, kwani huwezi kusimamia sheria wakati hutendi haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles