Na JUDITH NYANGE-MWANZA
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua wahalifu kwa kutoa taarifa kwa jeshi hilo zitakazowezesha kukamatwa kwao.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kumalizika kwa hafla ya kuwatunuku vyeti na zawadi askari polisi 30 wa Mkoa wa Mwanza waliofanya vizuri mwaka jana, Mangu alisema kazi ya kupambana na uhalifu inahitaji ushirikiano wa kila mtu.
Alisema ili kufanikisha kazi hiyo ni vema wananchi wakaendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi kwa siri.
"Kazi ya kupambana na uhalifu inahitaji usiri, ujasiri mkubwa na ushirikiano wa kila mtu, kama wananchi hawaamini baadhi ya askari ni vema wakatoa taarifa hizo kwa viongozi wao, " alisema Mangu.
Mangu alisema vita ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya inayoendelea nchini inahitaji askari wenye siri na ujasiri, ili kufanikisha kukamata mitandao wa wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo.
"Sitasita kuwachukulia hatua askari watakaokiuka maadili ya Jeshi la Polisi katika vita hii ya kupambana na dawa za kulevya kwa kuwaondoa.
"Najua kwenye msafara wa mamba kenge nao hawakosekani naomba wananchi watupatie taarifa za mienendo ya askari polisi ambao wanakwenda kinyume na maadili ya jeshi la polisi ili tuweze kuwachukulia hatua, "alisema Mangu.
Alisema suala la kuwepo kwa mashamba makubwa ya bangi katika maeneo mbalimbali linatokana na wananchi kukosa ushirikiano na jeshi hilo kwa kuwa hayajifichi na wao wanafahamu kuwepo wake katika maeneo yao.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amewapongeza wananchi kwa kuwapatia taarifa sahihi ambazo wao huzifanyia kazi na kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu wa makosa mbalimbali.