Na Brighiter Masaki,Mtanzania Digital
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia huru Mchekeshaji Idrisa Sultan(27) na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kurusha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Sultani ameachiwa huru na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Rubologa baada ya wakili wa Serikali Neema Mushi kudai kuwa DPP amewasilisha Nolle chini ya kifungu cha 91(1) cha CPA kuonesha kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Hakimu Rubologa amesema kwa kuwa DPP ameona hana nia ya kuendelea na kesi hiyo, mahakama yake inakubali ombi la Jamhuri inawaachia huru washtakiwa.
Mbali na Idrisa, washtakiwa wengine ni Doctor Ulimwengu(28) na Isihaka Mwinyimvua(22).
Katika kesi hiyo inadaiwa kati ya Machi 8, 2016 na Machi 12, 2020 sehemu tofauti tofauti jijini Dar es Salaam washitakiwa hao, walirusha maudhui online tv kwenye akaunti ijulikanayo Loko Motion bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini( TCRA).