Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MSANII wa vichekesho Idris Sultani na mwenzake wameachiwa huru baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta shahidi zaidi ya mara mbili.
Uamuzi huo wa kuwaachia huru umetolewa leo saa nne asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.
Sultan anakabiliwa na tuhuma ya kushindwa kusajili laini ya simu inayomilikiwa na mtu mwingine na mwenzake Innocent Maiga anashtakiwa kwa kushindwa kutoa taarifa.
Wakili wa Serikali Silvia Mitanto alidai kesi hiyo leo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini hawana shahidi sababu siku ya tarehe ya kesi Mei 14 ilikuwa sikukuu ya Eid.
Wakili wa utetezi, Jebra Kambole amepinga hoja hiyo kwa madai kwamba haina msingi, shauri la muda mrefu hivyo aliomba wateja wake waachiwe huru.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Chaungu alisema sababu ya upande wa Jamhuri haina msingi na kwamba Februari 22 mwaka huu alitoa ahirisho la mwisho, tangu hapo hakuna shahidi hadi Aprili 29, mwaka huu ambapo pia hawakuwa na shahidi.
“Kwa mazingira hayo mahakama inalifuta shauri hili chini ya kifungu cha sheria namba 225 , washtakiwa wanaachiwa huru,” alimesema na kuwaachia huru washtakiwa.
Hata hivyo washtakiwa hao bado wako chini ya ulinzi wa Polisi wakisuri maelekezo mengine kama yatakuwepo.
Maiga anakabiliwa na kosa la kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya matumizi ya laini ya simu kwa mtoa leseni kosa analodaiwa kulitenda kati ya Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020 katika eneo la Mbezi beach Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.