26.1 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Idara ya ardhi Dar yavunjwa

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAA



WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameivunja idara ya ardhi ya jiji la Dar as Salaam na kuagiza watumishi wote wa idara hiyo kuhamia wizarani.
Lukuvi alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za jiji hilo na kufanya ukaguzi katika masijala.

“Tangu 2015 nimeanza kazi wizara hii nimekuwa napambana na matapeli na wadanganyifu wa ardhi katika mkoa huu wa Dar es Salaam, leo nimefikia tamati.

“Chimbuko la udanganyifu mkubwa unatoka katika ofisi za jiji hasa maeneo ya Mbezi.
“Huko nyaraka za jiji ndizo zinazosababisha matatizo na mnajua kwamba jiji hili ni tofauti na majiji mengine, lenyewe halina ardhi, halipimi, halikusanyi kodi lakini majiji mengine, Arusha, Dodoma, Mwanza na Tanga yanafanya.

“Lakini bado linaendelea kutoa ofa za nyaraka za umiliki ardhi ambazo kwa msingi si halali,” alisema.
Waziri Lukuvi alisema nyaraka hizo zimekuwa zikisumbua kila siku wizarani akisisitiza kwamba huenda hazitolewi na jiji bali kuna matapeli wanaotumia mwanya huo mtaani.
“Hii niliyoshika ni feki, (akionyesha waandishi)…jiji halina mamlaka, nyaraka hii imetoka lakini kiwanja kina hati halali, ofa za jiji zinatumika kama halali.

“Kuanzia sasa mtu yeyote mwenye ofa ya namna hii haitatambulika ikiwezekana wakazibadilishe kwa kufuata utaratibu uliopo, nasi tutatambua tu iwapo ni kiwanja halali ama la,” alisisitiza.
Lukuvi aliwataka wataalamu wote wa ardhi wa jiji hilo wasitambue nyaraka hizo za ofa zilizopigwa muhuri wa jiji.

“Kuna watu wamekaa mkao wa kula hapa Dar kwa kutumia nyaraka hizi za ofa kutapeli wananchi, kuanzia sasa marufuku nyaraka hizi kutumika, nilishawaeleza wananchi miaka miwili iliyopita wananchi wazibadili.

“Mtu yeyote asinunue kiwanja chenye nyaraka ya ofa nchi nzima, serikali sasa inatoa hati,” alisema.
Aliongeza: “Kuanzia kesho (leo) watumishi hawa wataripoti ofisi ya kanda wizarani na nawataka maofisa ardhi wote wa manispaa kufika ofisi hizo za jiji kuchambua nyaraka zinazohusiana na kila wilaya, kumbukumbu ikakae huko.

“Kusiwe na mkanganyiko kwa sababu tunataka ikifika Desemba, mwaka huu tutaingiza nyaraka zote hizi katika mfumo wa elektroniki,” alisema.
Aliongeza: “Nimekuja kumtua mzigo Mkurugenzi wa Jiji asije akaingizwa kwenye mtego huu wa utapeli unaofanywa na wajanja.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Jiji la Dar as Salaam, Sporah Lyana alisema alibaini changamoto hiyo na kuanza kuzichambua nyaraka hizo na kuziweka kwenye makasha maalum.
“Tulianza kuzifungasha tangu Septemba, mwaka huu kuvitambua, tukashauriana tuandike na kuomba idhini mafaili haya yapelekwe kila manispaa,” alisema.
Awali, Waziri Lukuvi akizungumza maofisa ardhi wa wilaya za jiji hilo, alisema serikali inakusudia kuvichukua viwanja vyote ambavyo wahusika hawajaviendeleza katika mradi wa viwanja 20,000.
“Huu ni mradi mkubwa ambao ulisimamiwa na Wizara, huko maeneo ya Kibada, Gezaulole, Mwongozo, Buyuni, Mwanagati, Mbweni Malindi, Mbweni JKT, Mbweni Mpiji, Bunju na Twangoma.

“Vilipimwa viwanja hivyo lakini hadi leo zaidi ya asilimia 50 havijaendelezwa, havijajengwa, ni mradi wa miaka 10 iliyopita.
“Niliunda timu na kugundua baadhi viliwekwa majina bandia, havina wenyewe na wengine walinunua pengine wamesahau.

“Nimetoa maagizo maofisa ardhi wa wilaya wafanye ukaguzi wa mwisho, yeyote aliyenunua ikiwa hataweka japo ukuta, kufikia Desemba kiwanja hicho kirudishwe serikalini,” alisema.
Alisema zipo pia hati 6000 ambazo wenyewe hawajaenda kuzichukua hivyo amewaagiza maofisa hao kuzikagua kiwanja baada ya kiwanja.

“Hizi hati zipo hapa na serikali haipati kodi ya ardhi, serikali inapoteza fedha, tunaamini baadhi ya wafanyakazi wa ardhi waliopima vile viwanja waliweka majina bandia, tutavichukua viwanja vile na kuviuza tena,” alisema.
Alisema hati hizo zilitolewa na wizara zaidi ya miaka 10 iliyopita na hazijachukuliwa na zote ni za mkoa wa Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles